Mshukiwa mkuu wa mashambulizi ya kigaidi Barcelona auawa
Polisi ya Uhispania imemuua Younes Abouyaaqoub aliyetekeza shambulio la kigaidi la Alkhamisi wiki iliyopita katika mji wa Barcelona.
Vyombo vya habari vya Uhispania vimetangaza kuwa, mshukiwa huyo alipigwa risasi eneo la Subirats, karibu na Sant Sadurní d'Anoia lililoko umbali wa kilomita 60 kutoka Barcelona na alionekana kuvaa mkanda wa kujilipua.
Polisi wamethibitisha kwamba mshukiwa huyo ni Younes Abouyaaqoub, 22, ambaye awali alikuwa akisakwa kuhusiana na shambulio hilo la Las Ramblas.
Abouyaaqoub alikuwa akisakwa na polisi ya Uhispania tangu Alkhamisi iliyopita baada ya kuua watu 13 kwa kuwakanyaga kwa makusudi kwa gari katikati ya mji mwa Barcelona na kutoroka.
Baada ya mauaji ya watu katika mtaa wa Las Ramblas, Younes Abouyaaqoub aliteka gari jingine baada ya kumdunga kisu na kumuua dereva wake na kutoroka nalo hadi alikouliwa mafichoni.
Polisi ya Uhispania imetangaza kuwa, ingali inawasaka washukiwa wengine waliohusika na mashambulizi mawaili ya wiki iliyopita katika mji wa Barcelona. Watu 15 waliuawa katika mashambulizi hayo.
Kundi la kigaidi la Daesh limetangaza kuwa, ndilo lililopanga mashambulizi hayo.