Sep 02, 2017 15:02 UTC
  • Mahujaji wa Nyumba Tukufu ya Allah waendelea na amali za Hija

Zaidi ya mahujaji milioni moja wanaendelea na amali tukufu za Hija katika mji mtakatifu wa Makkah nchini Saudi Arabia.

Leo Jumamosi ambayo inasadifiana na mwezi 11 Mfunguo Tatu, siku ya pili ya Idul Adh'ha, mamia ya maelfu ya mahujaji wameendelea na amali za Hija baada ya kupitisha usiku wao wa kwanza huko Mina.

Leo mahujaji watalala tena Mina kabla ya kumpiga tena mawe shetani katika siku ya tatu ya idi. Baada ya hapo wataelekea Makkah kwa ajili ya kukamilisha amali zilizobakia za Hija.

Waislamu kutoka kona zote za dunia wakitufu al Kaaba

 

Mahujaji wametekeleza nguzo tano kuu za Hija yaani kusimama Arafa baadaye kulala Muzdalifa na halafu kuingia katika ardhi ya Mina asubuhi ya sikukuu ya Idul Adh'ha na baadae kumpiga mawe shetani na kuchinja mnyama pamoja na kunyoa nywele. Baada ya kukamilisha ibada zote za Hija, mahujaji wataelekea katika mji mtakatifu wa Madina kwa ajili ya kumzuru Bwana Mtume Muhammad SAW kwa wale ambao hawakufanya ziara hiyo kabla ya kuanza amali za Hija.

Kwa mujibu wa vyombo rasmi vya Saudi Arabia, idadi ya mahujaji mwaka huu imeongezeka sana ikilinganishwa na Hija ya mwaka jana ingawa hata hivyo na kutokana na siasa za Riyadh, Waislamu wa maeneo mbalimbali kama vile Syria, Yemen, Qatar n.k, wameshindwa kutekeleza ibada hiyo tukufu mwaka huu.

Tags