Sep 30, 2017 16:43 UTC
  • Waislamu wa madhehebu ya Shia leo wanaadhimisha siku ya Tasu'a

Waislamu wa madhehebu ya Shia na wapenzi wa watu wa familia ya Mtume Muhammad (saw) kote duniani leo wanaadhimisha siku ya Tusu'a kabla ya siku ya Ashura aliyouawa shahidi ndani yake mjukuu wa Mtume Muhammad (saw), Imam Hussein bin Ali bin Abi Twalib (as).

Siku hiyo huadhimishwa kila mwaka tarehe 9 Mfunguo Nne Muharram kukumbuka mapambano ya Imam wa tatu wa Waislamu katika kizazi cha Mtume Muhammad (saw), Hussein bin Ali (as) na wafuasi wake 72 waliouawa shahidi na jeshi la mtawala dhalimu wa kipindi hicho, Yazid bin Muawiya katika vita vya Karbala mwaka 680.

Maadhimisho hayo hukusanya idadi kubwa ya mamilioni ya watu hususan wafuasi na wapenzi wa Ahlulbait wa Mtume katika vituo, kumbi za kidini na kijamii na mitaani kwa marasimu na shughuli maalumu.

Maombolezo ya Tasu'a huko Karbala, Iraq

Nchini Iran shughuli hiyo ambayo imewakuwakutanisha mamilioni ya Waislamu kote nchini huambatana na kugawa sadaka na chakula kwa watu. Mamilioni ya Waislamu wenye mavazi ya rangi nyeusi kama alama ya huzuni na majonzi leo wanaendelea kushiriki katika shughuli hiyo kote hapa nchini wengi miongoni mwao wakibubujikwa na machozi na kughariki kwenye huzuni kubwa kwa kukumbuka masaibu yaliyompata mjukuu wa Mtume Muhammad (saw), Imam Hussein (as) na wafuasi wake 72. Shughuli ya maombolezo na kukumbuka masaibu ya Imam Hussein (as) itafikia kileleni kesho tarehe 10 Muharram ambayo ni maarufu kwa jina la siku ya A'shura. 

Haram ya Abul Fadhl Abbas bin Ali (as), Karbala

Siku ya Tasu'a yaani tarehe 9 Mfunguo Nne Muharram pia inajulikana kama Siku ya Uaminifu na Mapambano ambayo inahusishwa na Abbas bin Ali, ndugu yake Imam Hussein, kwa kuzingatia jinsi alivyojitolea na kusabilia nafsi yake katika vita vya Karbala kwa ajili ya kilinda Uislamu na kizazi cha Mtume (saw).   

Tags