Mattis: Marekani haina budi kubakia katika makubaliano ya nyuklia ya Iran
https://parstoday.ir/sw/news/world-i35205-mattis_marekani_haina_budi_kubakia_katika_makubaliano_ya_nyuklia_ya_iran
Waziri wa Ulinzi wa Marekani amesema serikali ya Rais Donald Trump wa nchi hiyo haina chaguo jingine ghairi ya kubakia kwenye makubaliano ya nyuklia ya Iran.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Oct 04, 2017 04:19 UTC
  • Mattis: Marekani haina budi kubakia katika makubaliano ya nyuklia ya Iran

Waziri wa Ulinzi wa Marekani amesema serikali ya Rais Donald Trump wa nchi hiyo haina chaguo jingine ghairi ya kubakia kwenye makubaliano ya nyuklia ya Iran.

Jim Mattis aliyasema hayo jana Jumanne alipofika mbele ya kamati ya Seneti, matamshi ambayo yanaoneka kukinzana na msimamo wa Trump.

Alipoulizwa na kamati hiyo iwapo anaamini kuwa makubaliano hayo yanayofahamika kama JCPOA yana maslahi kwa taifa la Marekani, waziri huyo amejibu kwa kusema: "Ndio ninaamini hivyo".

Amesema Rais wa Marekani anafaa kutafakari suala la Washington kubakia kwenye makubaliano hayo ya kimataifa, yaliyosainiwa Julai 2015 mjini Vienna na kuanza kutekelezwa Januari mwaka jana 2016.

Trump akihutubia mkutano wa hivi karibuni wa UN, New York

Licha ya jamii ya kimataifa ukiwemo Umoja wa Ulaya kukiri kuwa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imetekeleza ahadi zake zote katika fremu ya makubaliano hayo, chini ya uangalizi na ufuatiliaji wa Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki IAEA, lakini Marekani imekuwa ikifanya kila linalowezekana kukwamisha makubaliano hayo ya kimataifa. 

Trump ambaye aliwahi kusema wakati wa kampeni kuwa, mapatano ya nyuklia ya Iran ni 'maafa  na mapatano mabaya zaidi duniani' na kuahidi kuyachana katika siku yake ya kwanza katika Ikulu ya White House, amekuwa akiyakashifu makubaliano hayo kila leo.

Hata hivyo, Federica Mogherini, Mkuu wa Sera za Nje wa Umoja wa Ulaya amekuwa akisisitiza mara kwa mara kuwa makubaliano ya nyuklia kati ya Iran na kundi la 5+1 hayawezi kubatilishwa na serikali moja kwa kuwa yana baraka kamili ya Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa.