Bwabwaja za Trump kabla ya kuchukua uamuzi kuhusu makubaliano ya JCPOA
Rais Donald Trump wa Marekani ambaye amekuwa akifanya jitihada za kuharibu makubaliano ya nyuklia ya Iran na kundi la 5+1 kwa kutumia fursa na mbinu zote, kwa mara nyingine tena amedai kuwa, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran haitekelezi makubaliano hayo.
Trump ambaye jana alikuwa akihutubia makamanda wa jeshi la Marekani katika ikulu ya White House alisema karibuni hivi atatangaza uamuzi wake wa kupasisha au kutopasisha ripoti kuhusu makubaliano ya nyuklia ya JCPOA. Trump amedai kuwa, "Marekani haiwezi kuruhusu Iran kuwa na silaha za nyuklia". Bila ya kuzingatia harakati za mashirika ya ujajusi ya Marekani za kuanzisha na kufadhili makundi ya kigaidi katika Mashariki ya Kati, Donald Trump amedai pia kwamba, Iran inaunga mkono ugaidi na imeeneza ukatili na mauaji katika eneo hilo!
Misimamo hiyo ya Trump mbali na kuwa imejaa vinyongo na ni kinyume cha ukweli wa mambo, inaonesha kuwa, kiongozi huyo wa Marekani na utawala wa Kizayuni wa Isarel wameshikwa na hasira na hamaki kutokana na maendeleo ya Iran kama nchi yenye nguvu na yenye taathira kubwa katika eneo la Mashariki ya Kati. Kwa hakika matamshi hayo ya Trump ambayo yanafanana sana na yale aliyotoa katika mkutano wa 72 wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, yanaakisi kuchanganyikiwa kwa serikali ya sasa ya Marekani.
Akijibu matamshi ya kijinga ya Trump dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu, Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu Ayatullah Ali Khamenei alisema: "Matamshi yaliyotolewa na Donald Trump katika Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa hayalipi fakhari taifa la Marekani, na wasomi wa nchi hiyo wanapaswa kuona aibu kwa matamshi kama hayo na kutokana na kuwa na rais kama huyo." Alisema kuwa: "Matamshi hayo hayakutokana na nguvu bali yametokana na ghadhabu, kuchanganyikiwa na akili finyu".
Matamshi ya sasa ya Rais wa Marekani yanatathminiwa kuwa ni katika jitihada za kutayarisha mazingira ya kuchukua maamuzi mapya kuhusu makubalianio ya nyuklia ya JCPOA. Walimwengu na wafuatiliaji wa mambo wanaelewa kwa, Iran iko katika kambi inayopambana bila ya huruma na ugaidi na inakabiliana kwa hali na mali na magaidi wanaoungwa mkono na kusaidiwa na Marekani katika eneo la Mashaiki ya Kati kwa ajili ya kudumisha usalama na amani katika eneo hilo. Hivyo, bwabwaja za Donald Trump sawa kabisa na swahiba wake, Benjamin Netanyahu Waziri Mkuu wa utawala haramu wa Israel haziwezi kubadili uhakika na ukweli wa mambo.
Mikakati ya Trump ya kutaka kutayarisha mazingira kabla ya kutolewa ripoti ya tatu ya Washington kuhusu kufungamana au kutofungamana Iran na makubaliano ya nyuklia ya JCPOA ni ishara kwamba, kiongozi huyo atadai kuwa Iran haijaheshimu makubaliano hayo. Ripoti ya tatu ya Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani kuhusu makubaliano hayo itatolewa tarehe 15 Oktoba. Hata hivyo na sambamba na makelele hayo ya kipropaganda kunashuhudiwa upinzani mkali ndani ya serikali ya Marekani kwenyewe dhidi ya msimamo huo wa Trump.
Gazeti la Washington Post limefuchua kwamba, Trump hataunga mkono mapatano ya nyuklia ya Iran katika ripoti hiyo. Iwapo serikali ya Trump itachukua msimamo huo, Kongresi ya Marekani itakuwa na siku 60 za kuanza tena kutekeleza vikwazo vinavyohusiana na nyuklia dhidi ya Iran. Hata hivyo harakati hizo za Trump zinapigwa hata na mawaziri wa serikali yake. Waziri wa Ulinzi wa Marekani, James Mattis amesisitiza kuwa, kulindwa makubaliano ya nyuklia ya Iran kuna maslahi kwa Marekani. Vilevile Mkuu wa majeshi ya nchi hiyo, Joseph Dunford ameunga mkono makubaliano hayo na kuthibitisha kuwa, Iran imeyatekeleza na kuyaheshimu. Seneta wa chama cha Democratic, Elizabeth Warren pia alitoa taarifa jana akimtahadharisha Donald Trump juu ya taathira mbaya za kukiuka makubaliano ya nyuklia ya kundi la 5+1 na Iran.