Wanawake Waislamu Quebec, Canada wapigwa marufuku kuvaa niqab
Jimbo la Quebec nchini Canada limepaisha sheria za kuwapiga marufuku wanawake Waislamu kuvaa Hijabu yenye kufunika uso mzima maarufu kama niqab wakiwa wanatumia huduma za umma.
Katika upigaji kura wa Jumatano, bunge la kieneo la Quebec lilipiga kura 65-51 na hivyo kuidhinisha sheria hiyo ambayo inawalazimu wakazi wa eneo hilo kutofunika nyuso zao wakati wanapokea au kutoa huduma za umma kama vile usafiri.
Pamoja na kuwa sheria hiyo haikutaja vazi maalumu, lakini wengi wameitafsiri kuwa ni yenye kuwazuia wanawake Waislamu kuvaa niqab au burqa ambazo ni kati ya Hijabu zinazotumiwa na baadhi ya wanawake.
Sheria hiyo inawalenga wafanyakazi wa sekta ya umma kama vile madaktari, wauguzi na walimu.
Mjumbe wa Baraza Kuu la Wanawake Waislamu Canada, Shaheen Ashraf amesema sheria hiyo inawalenga Waislamu katika jimbo la Quebec.
Hii si mara ya kwanza kwa wanawake Waislamu kupigwa marufuku kuvaa aina mbali mbali za Hijabu katika nchi za Magharibi.