Njama za Marekani za kukandamiza harakati ya ususiaji utawala wa Israel
Kufuatia kuimarika harakati ya Ulimwengu ya Ususiaji dhidi ya Israel maarufu kwa jina la BDS nchini Marekani, jimbo la Wisconsin nchini humo limejiunga na majimbo ambayo yamepiga marufuku utiwaji saini mikataba na mashirika ambayo yanaunga mkono harakati hiyo ya kususia Israel.
Hivi sasa karibu nusu ya majimbo yote 50 ya Marekani yamechukua hatua za kuunga mkono utawala haramu wa Israel kwa kuchukua hatua dhidi ya taasisi au mashirika yanayoususia utawala huo wa Tel Aviv.
Harakati ya BDS kwa Kiingereza, Boycott, Divestment and Sanctions, ilianzishwa na Wapalestina mwaka 2005 kwa lengo la kuususia utawala wa Kizayuni wa Israel ili kuulazimisha utawala huo ghasibu uzingatie haki za taifa la Palestina na utii sheria za kimataifa.
Harakati hii imetangaza malengo yake manne makuu kuwa ni, kuushurutisha utawala wa Kizayuni usitishe ukaliaji mabavu wa ardhi za Palestina, kusitisha ujenzi wa vitongoji vya walowezi wa Kizayuni katika ardhi za Palestina, kupewa haki sawa Waarabu ambao ni raia wa utawala wa Israel na mwisho kupewa haki ya kurejea katika ardhi zao za jadi mamilioni ya wakimbizi wa Palestina.
Katika kipindi cha miaka 12, harakati hiyo imeweza kupata uungaji mkono mkubwa kote duniani ikiwa ni pamoja na ndani ya Marekani. Baadhi ya taasisi za kiraia, mashirika ya kibiashara, vyuo vikuu na vituo vya kiutamaduni vimetangaza kuunga mkono harakati hiyo ya kimataifa ya BDS ya kuisusia Israel.
Kwa mfano baadhi ya watu binafsi na mashirika yameamua kususia ushirikiano wowote na mashirika ya Israel au mashirika yanayounga mkono utawala huo ghasibu.

Wasusiaji wanaamini kuwa katika kukabiliana na utawala wa Kizayuni kunapaswa kutumiwa ile mbinu iliyotumiwa kuususia utawala wa ubaguzi wa rangi wa makaburu wa Afrika Kusini. Ususiaji huo hatimaye ulipelekea utawala huo wa makaburu ulegeze misimamo ya kibaguzi na kuwapa Waafrika wazalendo haki zao. Mbinu hii sasa inalenga kutumiwa dhidi ya utawala wa kibaguzi wa Israel ambao ubaguzi wake ni mbaya zaidi kuliko ule uliokuweko Afrika Kusini. Kuna matumaini kuwa mashinikizo ya kimataifa yataulazimisha utawala wa ubaguzi wa rangi wa Israel kulegeza misimamo na kuwarejeshea Wapalestina haki zao. Imebainika kuwa utawala huo wa Kizayuni umepata hasara kubwa kutokana na ususiaji huo wa kimataifa na hivyo harakati hiyo inaweza kutumika kuendelea kuushinikiza utawala huo wa kibaguzi.
Hivi sasa hata baadhi ya vyuo vikuu vyenye itibari Marekani vimejiunga na harakati hiyo ya kuususia utawala huo. Kwa kuzingatia kuwa wanachuo na waliohitimu katika vyuo vikuu wana ushawishi katika jamii, wanaweza kuwa na taathira katika kushawishi jamii zao ziususie utawala wa Israel na hili ni jambo ambalo limewatia wasiwasi mkubwa wakuu wa utawala huo na waungaji mkono wao barani Ulaya na Marekani.
Waungaji mkono wa Israel sasa wanawataja wanaohusika na kampeni hiyo ya BDS kuwa eti ni watu wenye chuki dhidi ya Mayahudi na kutumia kisingizo hicho kuwakandamiza. Ni kwa msingi huo ndio serikali ya Marekani ikachukua hatua isiyo ya kawaida ya kukandamiza sauti yoyote yenye kupinga Israel. Katika fremu hiyo, Marekani imejiondoa katika Shirika la Umoja wa Mataifa la Sayansi, Elimu na Utamaduni, UNESCO, kwa kisingizio kuwa taasisi hiyo inaukosoa utawala wa Kizayuni wa Israel na kuulaani utawala huo kutokana na njama zake za kujaribu kubadilisha muundo wa kijamii na kihistoria wa Quds Tukufu.
Muelekeo huu wa kiuhasama wa Marekani dhidi ya harakati ya BDS nchini humo ni ukiukwaji wa misingi ya uhuru wa maoni na katiba ya nchi hiyo.
Kilicho wazi ni kuwa, mashinikizo kama hayo ya Washington an Tel Aviv hayawezi kusitisha harakati za ukombozi wa Palestina na harakati ya kimataifa ya kuususia utawala wa Kizayuni wa Israel.