Mahakama ya Uhispania yatengua 'uhuru' wa Catalonia
Mahakama ya Katiba nchini Uhispania imebatilisha azimio lililopasishwa na bunge la eneo la Catalonia la kutangaza uhuru wa eneo hilo Ijumaa iliyopita.
Mahakama ya Katiba ya Uhispania imetoa uamuzi huo wakati ambapo Rais wa Catalonia, Carles Puigdemont alikuwa anahutubia waandishi wa habari akiwa nchini Ubelgiji.
Puigdemont amesema hajakimbilia Ubelgiji kutafuta hifadhi ya kisiasa, bali anataka kuuonyesha ulimwengu namna mfumo wa sheria wa Uhispania ulivyojaa kasoro sambamba na taifa hilo kuwa na demokrasia dhaifu.
Ijumaa iliyopita, Bunge la Catalonia lilipitisha azimio na kuchukua uamuzi wa upande mmoja wa kujitangazia uhuru wa kujitenga na Uhispania.
Wabunge 70 kati ya 135 wa bunge la Catalonia walipiga kura za 'ndiyo', 10 za 'hapana' huku wabunge wawili wakiamua kutopiga kura kupitisha uamuzi wa kulitangazia uhuru kamili eneo hilo wa kujitenga na Uhispania. Wabunge wa upinzani walitoka nje ya kikao hicho kabla ya upigaji kura kulalamikia uamuzi huo.
Katika muda wa chini ya saa moja baada ya hatua hiyo, Baraza la Seneti la Uhispania lilifanya kikao siku hiyo hiyo ya Ijumaa na kupiga kura ya kupitisha utekelezaji wa kifungu cha 155 cha katiba ya nchi hiyo kinachoipa mamlaka serikali kuu ya kulinyang'anya eneo hilo mamlaka ya kujiendeshea mambo yake ili kuliweka chini ya mamlaka ya moja kwa moja ya serikali kuu ya Uhispania.
Bunge la Catalonia lilipasiaha azimio hilo la kujitangazia uhuru baada ya wakazi wa eneo hilo kupiga kura ya kutaka kujitenga na maeneo mengine ya Uhispania mnamo Oktoba 26.