Nov 06, 2017 03:34 UTC
  • Askari wa zamani auwa 27 kanisani Texas nchini Marekani, makumi wajeruhiwa

Watu wasiopungua 27 wameuawa na makumi ya wengine kujeruhiwa katika shambulizi lililofanywa na askari wa zamani wa kikosi cha Jeshi la Anga la Marekani dhidi ya watu waliokuwa kanisani katika mji wa Sutherland Springs jimboni Texas.

Afisa wa polisi ya Marekani, Konstebo Devin Keen anasema kuwa, watoto kadhaa na mwanamke mmoja mja mzito ni miongoni mwa wahanga wa shambulizi hilo waliokuwa na umri wa baina ya miaka 5 hadi 72.

 Mtekelezaji wa shambulizi hilo ametambuliwa kuwa askari wa zamani wa Jeshi la Anga la Marekani ambaye Wizara ya Ulinzi ya nchi hiyo, Pentagon imemtaja kuwa ni Devin Patrick Kelley. Katili huyo pia ameuawa kwa kupigwa risasi na polisi ya FBI.

Maafisa wa FBI, Texas Marekani

Shambulizi hilo lililolenga watu waliokuwa katika kanisa la First Baptist katika jimbo la Texas limetajwa kuwa kubwa zaidi kufanyika dhidi ya watu waliokuwa wakifanya ibada katika historia ya sasa ya Marekani na baya zaidi kuwahi kutokea katika historia ya jimbo hilo.

Watu 24 wameuawa ndani ya kanisa, wawili nje yake na mmoja amefariki dunia baadaye kutokana na majeraha ya risasi. 

Maelfu ya Wamarekani huuawa kila mwaka kutokana na mashambulizi na ufyatuaji ovyo wa risasi katika maeneo mbalimbali ya nchi hiyo. 

Tags