Wajerumani waandamana kupinga chokochoko za Marekani dhidi ya Korea Kaskazini
Raia wa Ujerumani wameandamana katika mji mkuu wa nchi Berlin hiyo kulalamikia kuongezeka mivutano kati ya Marekani na Korea Kaskazini.
Maandamano hayo yalifanyika Jumamosi ya jana ambapo sambamba na kuunda mnyororo wa watu, waandamanaji hao walipiga kambi pia mbele ya balozi za Marekani na Korea Kaskazini mjini Berlin huku wakitoa nara za kulalamikia ongezeko la mivutano kati ya nchi mbili hizo ambazo kwa muda sasa zimekuwa zikitunishiana misuli. Katika maandamano hayo, waandamanaji walibeba mfano wa pipa la takataka la nyuklia na bendera zenye jumbe mbalimbali zinazosema: "Leteni amani, sio vita". Kadhalika waandamanaji walishikilia midoli yenye sura za Rais Donald Trump wa Marekani na Kim Jong-un, Kiongozi wa Korea Kaskazini.
Mivutano kati ya Washington na Pyongyang, ilishtadi baada ya Trump kuingia madarakani katika Ikulu ya White House ambapo tangu wakati huo amekuwa akitoa matamshi ya vitisho dhidi ya nchi hiyo ya Asia. Viongozi wa Korea Kusini wanaamini kwamba kupenda makuu kwa Marekani katika kukabiliana na mzozo wa Korea Kaskazini, ndio kumepelekea kutofikiwa maendeleo katika mazungumzo na Pyongyang. Hayo yalisema hivi karibuni na Lim Sung-nam, Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Korea Kusini.