Mar 23, 2016 15:02 UTC
  • Marekani yaendelea kuiunga mkono Saudi Arabia

Mfalme Salman bin Abdul Aziz wa Saudi Arabia amefanya mazungumzo na ujumbe wa Congresi ya Marekani ambapo pande hizo mbili zimejadili hali ya Mashariki ya Kati husuan Yemen na Syria.

Katika miezi ya hivi karibuni kulikuwepo habari za kujitokeza hitilafu kati ya Saudi Arabia na Marekani lakini hapana shaka kuwa baada ya Israel, Saudi Arabia ndio muitifaki mkubwa zaidi wa serikali ya Washington katika eneo la Magharibi mwa Asia.

Katika kipindi cha miaka mitano ya hivi karibuni Saudi Arabia haikuridhia siasa za Marekani kuhusu dikteta wa zamani wa Misri, Hosni Mubarak, msimamo wa Washington wa kutofanya mashambulizi ya kijeshi dhidi ya jeshi la Syria na kuhitimishwa faili la nyuklia la Iran. Hivyo, ili kuweza kuvutia tena roho ya kipenzi chake, Marekani imeamua kunyamazia kimya mashambulizi na mauaji yanayofanywa na Saudi Arabia dhidi ya Waislamu wa Yemen, uhalifu wa Saudia nchini Iraq, uungaji mkono wa Riyadh kwa makundi ya kigaidi huko Syria na ukiukwaji mkubwa wa haki za binadamu ndani ya Saudia kwenyewe.

Marekani inaitumia Saudi Arabia kama mmoja wa watekelezaji wa vita vya niaba katika eneo la magharibi mwa Asia. Washington inawauzia silaha watawala wa kifalme wa Saudia na kutumia silaha hizo na fedha za mafuta za serikali ya Riyadh katika vita vinavyopaganwa kwa niaba yake katika nchi za Waislamu. Kwa kutumia siasa hizo, Washington inapeleka mbele sera na siasa zake katika nchi hizo bila ya kutoa hata ndururu au kupoteza askari mmoja. Kwa maneno mengine ni kuwa, thamani na matukufu ya kibinadamu na kidini yanachinjwa na kukatwa kichwa katika migongano ya maslahi ya Saudi Arabia na Marekani.

Kwa upande wao watawala wa kizazi cha Aal Saud wanatumia hali hiyo na dola za mafuta kudumisha sera zao katika eneo la magharibi mwa Asia. Watawala hao wanahesabiwa kuwa wafadhili na waungaji mkono wakubwa wa makundi ya kigaidi na wasaidizi nambari moja wa tawala wa kidikteta dhidi ya matakwa ya wananchi. Ukweli huo unaonekana waziwazi katika misaada ya Saudi Arabia kwa makundi ya kigadi kama Daesh huko Syria, Iraq, Yemen na hata Libya, mambo ambayo yanapewa baraka kwa kimya cha Marekani. Mashambulizi ya Aal Saud dhidi ya Waislamu wa Yemen hadi sasa yameua maelfu ya watu wasio na hatia na kuharibu miundombinu ya nchi hiyo. Vilevile mashambulizi hayo yamewalazimisha mamilioni ya Wayemen hususan wanawake na watoto kuwa wakimbizi. Mauaji hayo pia yananyamaziwa kimya bali hata kushajiishwa na Marekani kwa lengo la kulinda maslahi yake nchini Saudi Arabia.

Kwa sasa ujumbe wa Congresi ya Marekani umeenda Riyadh kutayarisha safari ya Rais Barack Obama anayetarajiwa kuitembelea Saudia tarehe 16 Aprili na kukutana na Mfalme Salman. Nukta muhimu kuhusu uhusiano wa kistratijia wa Saudi Arabia na Marekani ni kwamba baadhi ya wachambuzi wa mambo hususan wa Kimarekani wanaamini kuwa, Washington inapaswa kutazama upya uhusiano wake na Riyadh na kuishinikiza Saudia kutokana na rekodi yake mbaya ya ukiukaji mkubwa wa haki za binadamu na kuunga mkono makundi ya kigaidi.

Tags