FAO yataka kuweko juhudi za kupambana na tatizo la njaa ulimwenguni
(last modified Thu, 30 Nov 2017 03:44:22 GMT )
Nov 30, 2017 03:44 UTC
  • FAO yataka kuweko juhudi za kupambana na tatizo la njaa ulimwenguni

Shirika la Chakula na Kilimo la Umoja wa Mataifa (FAO) limetoa wito wa kuungwa mkono na kusaidiwa wazalishaji wadogo ili kukabiliana na tatizo la njaa ulimwenguni.

José Graziano da Silv, Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Chakula na Kilimo la Umoja wa Mataifa (FAO) lenye makao yake Rome Italia amesema kuwa, kuna udharura wa wakulima kuungwa mkono na kusaidiwa ili suala la kupambana na tatizo la njaa ulimwenguni liwezekane.

Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Chakula na Kilimo la Umoja wa Mataifa (FAO) amesema kuwa, hii leo tatizo kuu la njaa sio uhaba wa chakula bali kupata chakula na bidhaa za chakula ndilo tatizo kuu na  hivyo uwekezaji katika sekta ya kilimo hususan kilimo cha umwagiliaji ni jambo la dharura.

Shirika la Chakula na Kilimo la Umoja wa Mataifa (FAO)

Mwezi Septemba mwaka huu, Shirika la Chakula na Kilimo la Umoja wa Mataifa (FAO) lilitahadharisha kuhusiana na kuuongezeka idadi ya watu wanaokabiliwa na baa la njaa ulimwenguni.

Aidha mwezi uliopita, Shirika la Chakula na Kilimo la Umoja wa Mataifa (FAO) lilitangaza kuwa, mwenendo wa kuongezeka vifo vya watu na mifugo kutokana na njaa na ukame katika eneo la mashariki mwa Afrika unatia wasiwasi mkubwa. 

Kadhalika ripoti mpya ya taasisi  za Umoja wa Mataifa zinasema kuwa, mwaka uliopita 2016, watu zaidi ya milioni 815 walikumbwa na baa la njaa kote duniani, ikiwa ni ongezeko la watu milioni 38 ikilinganishwa na mwaka juzi wa 2015.

Tags