PLO: Kuuhamishia Quds ubalozi wa Marekani ni 'busu la mauti'
https://parstoday.ir/sw/news/world-i37203-plo_kuuhamishia_quds_ubalozi_wa_marekani_ni_'busu_la_mauti'
Mwakilishi wa Harakati ya Ukombozi wa Palestina (PLO) nchini Marekani ameonya kuhusu madhara ya mpango wa Washington wa kuuhamisha ubalozi wake mjini Tel Aviv na kuupeleka katika mji mtakatifu wa Quds.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Dec 05, 2017 04:31 UTC
  • PLO: Kuuhamishia Quds ubalozi wa Marekani ni 'busu la mauti'

Mwakilishi wa Harakati ya Ukombozi wa Palestina (PLO) nchini Marekani ameonya kuhusu madhara ya mpango wa Washington wa kuuhamisha ubalozi wake mjini Tel Aviv na kuupeleka katika mji mtakatifu wa Quds.

Husam Zomlot ametahadharisha kuwa, hatua hiyo iwapo itatekelezwa, ni sawa na busu la mauti kwa azma yoyote ya kujaribu kuupatia ufumbuzi mgogoro wa Mashariki ya Kati, haswa kadhia ya Israel na Palestina.

Amesema kitendo hicho kitakuwa na taathira hasi na pana, akisisitiza kuwa bila shaka PLO itatoa jibu la kistratejia na kisiasa. 

Mwakilishi wa Harakati ya Ukombozi wa Palestina (PLO) nchini Marekani amebainisha kuwa, hatua ya Washington kuuhamishia ubalozi wake kutoka Tel Aviv hadi Quds tukufu ambayo ni roho ya mgogoro wa Mashariki ya Kati, itaipotezea itibari Marekani ambayo inajifanya kuwa mpatanishi; na sasa itabainika wazi kuwa nchi hiyo ni sehemu ya matatizo na wala sio suluhu.

Mashariki mwa Quds Tukufu inayokaliwa kwa mabavu

Aidha hivi karibuni, wajumbe wa PLO huko Lebanon walitangaza katika taarifa yao kwamba, mpango wa Trump wa kuhamisha makao ya ubalozi wa nchi yake kutoka Tel Aviv na kuyapeleka huko Baytul Muqaddas ni ukiukaji wa wazi wa sheria na maazimio ya kimataifa.

Baadhi ya ripoti zinasema kuwa, kesho Jumatano, Rais Donald Trump wa Marekani anakusudia kutangaza kuutambua rasmi mji wa Quds kuwa mji mkuu wa utawala pandikizi wa Israel, sambamba na kuuhamishia ubalozi wa nchi hiyo mjini Quds, kutoka Tel Aviv.