UN: Serikali ya Myanmar inafanya mauaji ya kimbari dhidi ya Waislamu
https://parstoday.ir/sw/news/world-i37239-un_serikali_ya_myanmar_inafanya_mauaji_ya_kimbari_dhidi_ya_waislamu
Kamishna Mkuu wa Haki za Binadamu wa Umoja wa Mataifa amesema kuwa uhalifu unaofanywa na Mabudha nchini Myanmar dhidi ya Waislamu wa jamii ya Rohingya ni mauaji ya kimbari.
(last modified 2025-11-07T02:31:33+00:00 )
Dec 06, 2017 04:53 UTC
  • UN: Serikali ya Myanmar inafanya mauaji ya kimbari dhidi ya Waislamu

Kamishna Mkuu wa Haki za Binadamu wa Umoja wa Mataifa amesema kuwa uhalifu unaofanywa na Mabudha nchini Myanmar dhidi ya Waislamu wa jamii ya Rohingya ni mauaji ya kimbari.

Zeid Ra'ad Al Hussein amesisitiza katika kikao cha Baraza la Haki za Binadamu la Umoja wa Mataifa lililokutana kujadili hali ya Waislamu wa Rohingya katika jimbo la Rakhine huko Myanmar kwamba, kuna udharura wa kufika katika maeneo mbalimbali ya nchi hiyo na kufanya uchunguzi kuhusu ukatili unaofanywa na serikali ya Myanmar dhidi ya Waislamu. 

Kamishna Mkuu wa Haki za Binadamu wa Umoja wa Mataifa amesema kuwa kutotambua haki za watu wa jamii ya Rohingya kama kaumu yenye haki na heshima ni kuwadunisha na kuwadhalilisha Waislamu wa Myanmar. 

Ra'ad Al Hussein amesema kuwa, Waislamu wa Rohingya wanalengwa na kuuawa kwa sababu ya utambulisho wao na kwamba wananyimwa hata haki ya kuwa na majina ya Kiislamu. 

Hata watoto wadogo wanauawa Myanmar

Wakati huo huo Baraza la Haki za Binadamu la Umoja wa Mataifa limetoa azimio likiitaka serikali ya Myanmar kuwaruhusu wataalamu wa umoja huo kuchunguza jinai na uhalifu unaofanyika dhidi ya Waislamu wa Rohinya nchini humo. 

Azimio hilo pia limeitaka serikali ya Myanmar kukomesha ukatili na mauaji dhidi ya Waislamu. 

Maelfu ya Waislamu wa kabila la Rohingya nchini Myanmar wameuawa na maelfu ya wengine kujeruhiwa tangu kuanza wimbi jipya la mashambulizi ya jeshi na Mabudha wenye misimamo mikali katika mkoa wa Rakhine magharibi mwa nchi nchi hiyo tarehe 25 Agosti mwaka huu. 

Wanawake wa Kiislamu wanabakwa nchini Myanmar

Vilevile shirika la kutetea haki za binadamu la Human Rights Watch (HRW) limesema jeshi la Myanmar linawaua kiholela na kuwanajisi wanawake Waislamu wa jamii ya Rohingya magharibi mwa nchi hiyo.