Kituo cha Kiislamu nchini Sweden chapigwa bomu na magaidi wanaopinga Uislamu
https://parstoday.ir/sw/news/world-i38153-kituo_cha_kiislamu_nchini_sweden_chapigwa_bomu_na_magaidi_wanaopinga_uislamu
Duru za habari nchini Sweden zimetangaza kuwa, kituo cha Kiislamu nchini humo kimeshambuliwa kwa bomu la kutengenezwa kwa mkono.
(last modified 2023-11-27T12:14:11+00:00 )
Dec 27, 2017 02:41 UTC
  • Kituo cha Kiislamu nchini Sweden chapigwa bomu na magaidi wanaopinga Uislamu

Duru za habari nchini Sweden zimetangaza kuwa, kituo cha Kiislamu nchini humo kimeshambuliwa kwa bomu la kutengenezwa kwa mkono.

Abd Hakem Aden, mkuu wa kituo hicho cha Kiislamu nchini Sweden amesema kuwa, shambulizi hilo lilitokea Jumanne ya jana na kwamba lilisababisha hasara kubwa ikiwemo kuharibiwa milango na madirisha yake. Ameongeza kwa kusema kuwa, shambulizi hilo la kutisha limeathiri pia kuta za msikiti wa eneo hilo.

Miongoni mwa hujuma za kigaidi dhidi ya Waislamu nchini Sweden

Polisi ya Sweden imetangaza kuanza uchunguzi kuhusiana na shambulio hilo ingawa uchunguzi wa mwanzo unaonyesha kuwa, hujuma hiyo imefanywa kwa makusudi na genge la watu wenye chuki dhidi ya Waislamu.

Kabla ya hapo pia kituo kingine cha Kiislamu cha Imamu Ali (as) nchini Sweden ambacho kinajumuisha msikiti mkubwa wa Waislamu wa madhehebu ya Shia kilichomwa moto na watu wenye misimamo ya kigaidi. Kufuatia tukio hilo Ayatullah Muhsin Hakim Ilahi, mkuu wa kituo hicho cha Imamu Ali Ibn Abi Twalib (as) alisema kuwa shambulio hilo lilitokana na uzembe wa polisi ya nchi hiyo kwa kuacha kutoa ulinzi wa kuzuia magenge ya kigaidi yanayoendesha kampeni za chuki dhidi ya Uislamu na Waislamu.

Mashambulizi hayo yanawalenga Waislamu wote

Kuongezeka kwa wimbi la chuki na ubaguzi dhidi ya Uislamu katika nchi za Magharibi ikwemo Sweden, kumewasababishia wasiwasi mkubwa wafuasi wa dini hiyo. Wimbi hilo la chuki lilishika kasi zaidi baada ya Rais Donald Trump wa Marekani kushika hatamu za uongozi, ambapo Waislamu wa nchi za Magharibi wamekuwa wakiandamwa na hujuma hizo zinazoambatana na ubaguzi.