Iran, Russia zalitaka Baraza la Usalama lisifuate mashinikizo ya Marekani
Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na Russia zimekosoa udhaifu wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa wa kukubali mashinikizo ya Marekani ya kuitisha kikao cha dharura kuhusu maandamano ya hivi karibu nchini Iran.
Gholamali Khoshroo, Balozi wa Iran katika Umoja wa Mataifa jana Ijumaa alikiambia kikao hicho cha Baraza la Usalama kuwa, amesikitika kuliona baraza hilo likiburuzwa na Marekani kuitisha mkutano wa kujadili kadhia ambayo ni ya ndani ya Iran.
Amesema Marekani haina itibari ya kisiasa wala kimaadili machoni pa dunia, na kwamba kitendo hicho cha Marekani kinatokana na ukosefu wa ufahamu wa sera za kigeni wa Rais Donald Trump.
Kwa upande wake, Balozi wa Ufaransa katika Umoja wa Mataifa, Francois Delattre amesema maandamano nchini Iran hayahatarishi usalama wala amani ya dunia huku akieleza hofu yake ya kutumiwa mgogoro huo kwa 'maslahi binafsi'.
Naye Vasily Nebenzia, Balozi wa Russia UN ameikosoa vikali Washington kwa kujaribu kupindisha majukumu ya Baraza la Usalama, akisisitiza kuwa, maandamano ya Iran ni tatizo la ndani ambalo litapatiwa ufumbuzi na viongozi husika wa nchi hiyo.
Wananchi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran baada ya Sala ya Ijumaa hapo jana walishiriki kwenye maandamano makubwa katika maeneo mbalimbali nchini, ukiwemo mji mkuu Tehran, kulaani fujo na ghasia zilizozushwa hivi karibuni huku wakitaka wahusika wa fitina hiyo wachukuliwe hatua kali kisheria.