Waziri Mkuu wa Hungary awaita wakimbizi Waislamu 'wavamizi'
Waziri Mkuu wa Hungary amewataja wakimbizi Waislamu wanaowasili katika nchi za Ulaya wakikimbia migogoro Mashariki ya Kati na Kaskazini mwa Afrika kuwa 'wavamizi Waislamu'.
Katika mahojiano na gazeti la Ujerumani la Bild, Viktor Orban amesema 'Hawa watu hatuwatambui kama wakimbizi Waislamu, bali tunawatizama kama wavamizi waliopata ujasiri wa kuja barani hapa kwa sababu za kiuchumu.'
Amesema jitihada za kutaka wanadamu watangamane pasina kujali dini zao ni njozi, na kwamba jamii za Wakristo na Waislamu katu haziwezi kuungana.
Waziri Mkuu huyo wa Hungary mwenye misimamo ya chuki dhidi ya Uislamu, Waislamu na wakimbizi amewahi kunukuliwa na vyombo vya habari akisema kuwa wahajiri ni kirusi hatari cha ugaidi barani Ulaya.
Kwa mujibu wa takwimu za Shirika la Kuhudumia Wakimbizi la Umoja wa Mataifa (UNHCR), watu zaidi ya milioni mbili walilazimika kuwa wakimbizi katika maeneo mbalimbali duniani mwaka jana 2017.
Mapigano, machafuko, mauaji na vitendo vya maudhi na hujuma katika nchi za Myanmar, Sudan Kusini, Syria na katika nchi nyingine kama Yemen na kwingineko vimewafanya raia wa nchi hizo kuyakimbia makazi yao na kuomba hifadhi katika nchi nyingine.