Zaidi ya watu 50 wauawa katika mripuko wa bomu Pakistan
-
Mripuko Pakistan
Kwa akali watu 52 wameuawa na makumi ya wengine kujeruhiwa kwenye mripuko wa bomu uliotikisa mji wa Lahore, kaskazini mashariki mwa Pakistan.
Polisi ya Pakistan imesema mripuko huo wa jana Jumapili ulitokea nje ya Bustani ya Gulshan Iqbal mjini Lahore, katika mkoa wa Punjab, ambao ni moja ya mikoa salama isiyoshuhudia hujuma za kigaidi. Hata hivyo taarifa ya polisi ya nchi hiyo haijafafanua iwapo mripuko huo wa bomu ni hujuma ya kigaidi au la. Hakuna kundi lolote la kigaidi lililokiri kuhusika kwenye hujuma hiyo, ingawa kundi la kigaidi na kitakfiri la Taliban limekuwa likifanya mashambulio ya aina hii nchini humo.
Jam Sajjad Husein, mmoja wa maafisa wa uokoaji amesema aghalabu ya waliojeruhiwa katika mripuko huo wa bomu ni wanawake na watoto wadogo.
Hivi karibuni, watu zaidi ya 17 waliuawa katika shambulio la bomu lililolenga basi la wafanyakazi wa serikali katika mkoa wa Khaybar Pakhtunkhwa, karibu na mpaka na Afghanistan.
Aidha mwezi Januari mwaka huu, watu 15 waliripotiwa kuuawa na wengine zaidi ya 20 walijeruhiwa katika shambulio la bomu lililolenga maafisa wa usalama nje ya kituo cha utoaji chanjo ya ugonjwa wa kupooza (polio) mjini Quetta huko kusini magharibi mwa Pakistan.