Russia: Ushahidi uliotolewa na Marekani dhidi ya Iran ni butu
Russia imesema kuwa ushahidi uliotolewa na Marekani ikidai kuwa Tehran imewapa makombora wapiganaji wa harakati ya al Huothi nchini Yemen ni butu na hauna mashiko.
Balozi wa Russia katika Umoja wa Mataifa, Vassily Nebenzia ambaye alipelekwa Washington pamoja na wanadiplomasia wengine wa Baraza la Usalama kuoneshwa kinachodaiwa ni mabaki ya makombora ya Iran yalioyotumiwa na wapiganaji wa Ansarullah huko Yemen dhidi ya Saudi Arabia, amesema kuwa Iran inakanusha kwa nguvu zote kwamba inatuma silaha nchini Yemen.
Balozi wa Russia katika Umoja wa Mataifa amesisitiza kuwa, Yemen ina silaha nyingi za miaka iliyopita na kwa msingi huo hawezi kutoa maoni kuhusu silaha zilizoko nchini humo na kwamba hakuna hatua yoyote itakayochukuliwa dhidi ya Iran katika Umoja wa Mataifa kutokana na madai hayo ya Marekani.
Siku kadhaa zilizopita balozi wa Marekani katika Umoja wa Mataifa, Nikki Haley aliwaalika chakula cha mchana mabalozi wa nchi wanachama wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa mjini Washington kwa lengo la kuwaonesha kipande cha chuma ambacho Marekani inadai ni mabaki ya kombora la Iran lililovurumishwa nchini Saudi Arabia na Ansarullah ya Yemen.
Haley alidai kuwa chuma hicho kinachodaiwa ni mabaki ya kombora la Iran kinaonyesha kwamba Tehran inakiuka sheria ya kimataifa kwa kuipa makombora harakati ya Houthi nchini Yemen.
Balizo wa Iran katika Umoja wa Mataifa umekanusha madai hayo ya Marekani akisisitiza kuwa hayana na misingi. Amesema kuwa madai hayo yanatolewa kwa shabaha ya kuficha uhalifu wa kivita wa Saudi Arabia ikishirikiana wa Marekani nchini Yemen na kuwasahaulisha walimwengu maafa yanayosababishwa vita vya kikatili dhidi ya watu wa Yemen.