Russia: Suala la kuangaliwa upya makubaliano ya JCPOA halipo
Balozi na mwakilishi wa kudumu wa Russia katika Umoja wa Mataifa amesema kuwa, suala la kuangalia upya makubaliano ya nyuklia ya JCPOA halipo.
Akizungumza katika mahojiano aliyofanyiwa na kanali ya televisheni ya Russia 24 Vasily Nabenzya amesisitiza kwamba, hakuna kabisa uwezekano wa kutazama upya makubaliano hayo yaliyofikiwa kati ya Iran na kundi la 5+1 na kuidhinishwa na Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa.
Sergei Lavrov, Waziri wa Mashauri ya Kigeni ya Russia amesisitiza pia kwamba, njama za kutaka kuyavuruga makubaliano hayo yanayojulikana kama Mpango Kamili wa Pamoja wa Utekelezaji JCPOA kwa kifupi, zitakuwa na gharama kubwa.
Lavrov amezitaka pande zote husika kushikamana kikamilifu na makubaliano hayo ya kimataifa ambayo yalikuwa matunda ya mazungumzo marefu.
Waziri wa Mambo ya Nje wa Russia aidha ameonya kuwa kuvunjika makubaliano ya nyuklia na Iran kunaweza kuwa na matokeo yasiyoweza kutabirika.
Wakati huohuo Naibu Waziri wa Mashauri ya Kigeni ya Russia, Sergei Ryabkov, ametahadharisha kuwa, hatua za Marekani za kutaka hati ya JCPOA ifanyiwe mabadiliko mwishowe zitapelekea kusambaratika makubaliano hayo; na Moscow haitotaka kwa namna yoyote ile ihusike katika mchakato huo haribifu.
Mapatano ya nyuklia ya Iran na kundi la 5+1 ambazo ni nchi za Uingereza, Ufaransa, Russia, China, Marekani pamoja na Ujerumani yalianza kutekelezwa Januari 2016 lakini sasa Marekani inafanya juhudi za kutaka kuyavuruga.