Taarifa ya nchi nne za Magharibi dhidi ya Russia
Viongozi wa nchi za Uingereza, Ujerumani , Ufaransa na Marekani wametoa taarifa ya pamoja wakiibebesha Russia jukumu la kushambuliwa kwa mada za sumu Sergei Skripal, jasusi wa zamani wa Russia.
Taarifa hiyo iliyotolewa jana Alkhamisi inasema kuwa shambulio la aina hiyo ni la kwanza kuwahi kutekelezwa dhidi ya nchi ya Ulaya baada ya kumalizika Vita vya Pili vya Dunia, shambulizi ambalo linadaiwa kukiuka misingi ya kujitawala Uingereza pamoja na sheria za kimataifa zinazopiga marufuku matumizi ya silaha za kemikali. Mvutano wa pande mbili za Uingereza na Russia juu ya kushambuliwa Sergei Skripal na binti yake Yulia kwa mada za kemikali umebadilika na kuwa makabiliano makubwa kati ya nchi za Magharibi na Russia. Hujuma hiyo ya kisiasa na kipropaganda ambayo inaendeshwa na nchi za Magharibi dhidi ya Russia tena katika kipindi hiki ambacho nchi hiyo ya kambi ya Mashariki inajiandaa kufanya uchaguzi mkuu wa rais nchini, imevuruga zaidi hali ya mambo na kuna uwezekano wa kuharibika zaidi hali hiyo katika siku zijazo. Kuhusu mgogoro huo, viongozi wa Ungereza wamekanyaga misingi ya maadili na taratibu za kidiplomasia na kuishambulia Russia na viongozi wake kwa maneno makali na yasiyokuwa ya adabu.
Kuhusiana na suala hilo, jana Alkhamisi Gavin Williamson, Waziri wa Ulinzi wa Uingereza alisema kushambuliwa Sergei Skripal kwa mada za kemikali ni hatua ya jeuri kutoka kwa serikali ya Moscow na kuongteza kuwa badala ya Russia kutoa jibu kuhusiana na suala hilo ni bora isimame kando na kunyamaza kimya. Dharau hiyo ya viongozi wa Uingereza haikunyamaziwa na Warussia bali Igor Konashenkov, Msemaji wa Wizara ya Ulinzi ya Russia alitoa jibu kali kwa kusema kuwa matamshi hayo yasiyo na hadhi na ya mitaani ya Waziri wa Ulinzi wa Uingereza yanadhihirisha wazi udhaifu wake wa kiakili. Amesema: 'Matamshi hayo yote si tu kwamba yanabainisha kukosa thamani tuhuma zinazotolewa dhidi ya Russia bali pia yanaonyesha kutokuwa na thamani watu wanaozitoa tuhuma hizo.'
Kwa mtazamo wa Moscow, London imeanzisha mgogoro wa hivi sasa ili kufunika matatizo yake ya ndani. Theresa May, Waziri Mkuu wa Uingereza hayuko peke yake katika uwanja huo na taarifa ya pamoja iliyotolewa na viongozi wa nchi nyingine za Magharibi kuhusu mgogoro huo inabainisha wazi kwamba wameamua kuiunga mkono Uingereza katika mgogoro huo dhidi ya Russia.
Kwa hakika nchi hizo za Magharibi zimepata kisingizio kizuri kwa ajili ya kudhoofisha nafasi ya Russia kaika ngazi za kimataifa kwa kuituhumu kuwa ni nchi ya kwanza kutumia silaha za kemikali dhidi ya nchi za Ulaya baada ya kumalizika Vita vya Pili vya Dunia. Kwa kuzingatia hilo, tunataraji kuona mashinikizo ya kisiasa na kipropaganda ya nchi za Magharibi yakiongezeka dhidi ya Russia katika siku chache zijazo. Theresa May ndiye mwanzilishi wa hali hiyo. Siku ya Jumatano alikariri tuhuma za kuhusika Russia katika shambulio la mada za sumu dhidi ya Sergei Skripal na binti yake na hatimaye kutoa amri ya kufukuzwa nchini Uingereza wanadiploamasia 23 wa Russia. Alkhamisi, Wizara ya Fedha ya Marekani nayo ilifuata mkono huo wa kutolewa mashinikizo ya nchi za Magharibi dhidi ya Russia kwa kuwawekea vikwazo vipya raia na mashirika kadhaa ya Russia.
Licha ya kuboreka kwa kiwango fulani uhusiano wa Russia na Umoja wa Ulaya, kama vile mazungumzo ya hivi karibuni kati ya Rais Vladimir Putin wa Russia na viongozi wa nchi kadhaa za Ulaya akiwemo Emmanuel Macron wa Ufaransa, lakini matukio ya hivi karibuni katika uhusiano wa pande mbili za Moscow na Magharibi, bila shaka yatapelekea kupanuka zaidi ufa uliopo kati ya pande hizo na hivyo kuongeza mivutano na makabiliano baina yao katika nyanja tofauti za kisiasa, kidiplomasia, kiuchumi na kibiashara.