Russia yajibu mapigo kwa kuwatimua wanadiplomasia 23 wa Uingereza
Wizara ya Mambo ya Nje ya Russia imetangaza kuwa imewafukuza na kuwataka waondoke nchini humo wanadiplomasia 23 wa Uingereza kufuatia hatua kama hiyo iliyochukuliwa hivi karibuni na seriikali ya London dhidi ya wanadiplomasia wa Russia.
Kanali ya televisheni ya Russia Today imeripoti kuwa Wizara ya Mambo ya Nje ya Russia vilevile imeamua kusimamisha shughuli za kituo cha utamaduni cha Uingereza kilichoko mjini Moscow na kuufunga ubalozi mdogo wa nchi hiyo ulioko katika mji wa Saint Petersburg.
Uamuzi na hatua hizo zimechukuliwa katika hali ambayo, Wizara ya Mambo ya Nje ya Russia leo asubuhi imemwita kwa mara ya pili Laurie Bristow, balozi wa Uingereza mjini Moscow.
Sambamba na hayo, Wizara ya Mambo ya Nje ya Russia imeionya Uingereza kuwa ikiwa itachukua hatua yoyote mpya dhidi ya Russia, Moscow nayo itakuwa na haki ya kujibu mapigo kwa kuchukua sawa na hiyo dhidi ya London.
Waziri wa Mambo ya Nje wa Russia Sergei Lavrov alitangaza jana kuwa Moscow itajibu mapigo tu kwa kuwafukuza wanadiplomasia wa Uingereza kutokana na hatua sawa na hiyo iliyochukuliwa na serikali ya London hivi karibuni dhidi ya wanadiplomasia wa Russia.
Jumatano ya tarehe 14 Machi, Waziri Mkuu wa Uingereza Theresa May alitoa amri ya kufukuzwa wanadiplomasia 23 wa Russia baada ya kukariri madai kwamba serikali ya Moscow imehusika na tukio la kumpa sumu jasusi wa pande mbili mwenye asili ya Russia Sergei Skripal pamoja na binti yake Yulia ambao wote wawili walikumbwa na mkasa huo katika mji wa Salisbury, kusini mwa London, mji mkuu wa Uingereza. Jasusi huyo wa pande mbili mwenye umri wa miaka 66 na binti yake mwenye umri wa miaka 33 walikimbizwa hopsitalini baada ya kuzirai, na inasemekana kuwa hadi sasa hali zao ni mahututi.
Russia imekanusha tuhuma hizo zilizotolewa na Uingereza na kusisitiza kwamba serikali ya London imezusha tuhuma hizo kwa madhumuni ya kupotosha fikra za waliowengi duniani.../