Kikao cha kimataifa cha kupambana na magendo ya wahajiri huko Niger
Kikao cha kimataifa cha kupambana na magendo ya wahajiri kimefanyika huko Niger kwa kuhudhuriwa na viongozi wa nchi wanachama wa Umoja wa Afrika (AU) na wa nchi kadhaa za Ulaya. Mohammed Bazoum Waziri wa Mambo ya Ndani wa Niger amesema kwenye kikao hicho kuwa taathira za mapambano hayo zitaongezeka kwa kiasi kikubwa iwapo kutakuwepo mashirikiano ya kiusalama katika ngazi ya kitaifa na kieneo.
Kikao cha kimataifa cha kupambana na magendo ya wahajiri kimefanyika katika hali ambayo nchi za Kiafrika zinakabiliwa na matatizo mbalimbali katika nyanja za kisiasa, kiuchumi na kijamii khususan kuzorota hali ya kiuchumi, umaskini na ukosefu wa ajira; masuala yanayolipelekea bara hilo kukabiliwa na migogoro miwili mikubwa.
Mgogoro wa kwanza ni wimbi la wahamiaji haramu wanaojaribu kuelekea Ulaya kutokana na matatizo ya kiuchumi na ukosefu wa amani katika nchi zao; na wa pili ni kuongezeka vitisho vya makundi ya kigaidi barani Afrika. Aidha makundi mengi ya kigaidi yamekuwa yakisajili wanachama wapya kujiunga nayo kwa kuwaahidi kuwapatia misaada ya kifedha katika nchi za Kiafrika. Kwa msingi huo matatizo mawili yaani wahajiri haramu na kuenea ugaidi yamekuwa si tu hatari mbili kuu kwa bara la Afrika bali kwa bara Ulaya pia.
Kuhusu suala la wahajiri, ukosefu wa uthabiti wa kisiasa na kushindwa kudhibitiwa mipaka ya Libya ambayo imekuwa ikitumika kama njia kuu ya wahajiri kutoka katika bahari ya Mediterania kuelekea katika nchi za Ulaya pia kumezidisha wimbi la wahajiri wa Kiafrika. Hii ni katika hali ambayo wahajiri hao wanakabiliwa na masaibu na vikwazo mbalimbali katika safari zao hizo za kutaka kufika barani Ulaya. Kuwepo hatari ya magenge ya magendo ya binadamu, utumiaji mabavu, kutozwa fedha nyingi ili kuweza kusafirishwa hadi Ulaya na kutumiwa kama watumwa ni miongoni mwa mashaka na vizuizi wanavyokumbana navyo wahajiri hao wa Kiafrika.
Katika upande mwingine nchi za Ulaya pia kwa muda sasa zimekuwa zikitekeleza siasa kali dhidi ya wahajiri kukiwemo kufunga mipaka na kuwarejesha wahajiri katika nchi walikotoka. Hata wale wahajiri ambao wanafanikiwa kuingia Ulaya pia aghalabu yao hukumbwa na matatizo na mashaka chungu nzima. Guy Ryder Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Kazi Duniani (ILO) anasema kuhusu suala hilo kuwa: Wafanyakazi wengi wahajiri duniani ni wahanga wa vitendo vya ubaguzi, aina mbalimbali za unyanyasaji na utumiaji mabavu sehemu za kazi na wala hakuna uwezekano kwa kundi hilo kunufaika na msaada wa kimsingi kabisa wa kijamii na kiraia.
Kiujumla hali hii imezipelekea nchi za Ulaya kutekeleza siasa mbalimbali kama kutenga kiasi cha fedha kwa ajili ya kusaidia ustawi wa Afrika na kudhibiti wahajiri wanakotokea. Hii ni katika hali ambayo siasa hizo kivitendo ni nara tupu na hazitekelezwi kwa ajili ya kudhamini maslahi ya Afrika na watu wa bara hilo bali zimekusudiwa kudhamini maslahi ya nchi za Ulaya, kudhibiti wimbi la wahajiri na kile kinachotajwa kuwa ni mapambano dhidi ya kuenea ugaidi. Japokuwa hadi sasa vikao mbalimbali vimefanyika kati ya wakuu wa Ulaya na Afrika na katika kikao cha sasa huko Niger pia washiriki wametafuta suluhisho la tatizo lililopo na kuhakikisha kuwa bara la Afrika lina kuwa na usalama ili kuzuia kuendelea kuwepo wimbi la wahajiri, lakini inaonekana kuwa mgogoro wa wahajiri unaweza tu kupatiwa ufumbuzi iwapo kutaandaliwa na kuboreshwa miundo mbinu ya kiuchumi, kijamii na kisiasa katika nchi za Kiafrika kwa kuheshimu misingi ya usawa na uadilifu.