Iran, Russia, Uturuki zatoa tamko la pamoja kuhusu Syria
Mawaziri wa Mambo ya Nje wa Iran, Russia na Uturuki wametoa tamko la pamoja mwishoni mwa kikao chao cha mjini Moscow, Russia na kutilia mkazo wajibu wa kulindwa ardhi nzima ya Syria na haki ya kujitawala na kujiamulia lenyewe mambo yake taifa hilo la Kiarabu.
Nchi za Iran, Russia na Uturuki ndizo zenye dhamana ya mchakato wa kusimamishwa vita nchini Syria, na leo walikuwa na kikao cha pamoja mjini Moscow kujadili suala la Syria.
Nchi hizo tatu zimesisitizia msimamo wao wa kuendelea kushirikiana katika kuutafutia ufumbuzi wa kudumu mgogoro wa Syria katika kalibu ya tamko la pamoja lililotolewa na marais wa nchi hizo tatu tarehe 22 Novemba 2017 na tarehe 4 Aprili 2018.
Wakati huo huo mawaziri wa mambo ya nje wa nchi tatu za Iran, Russia na Uturuki wamesema katika tamko lao hilo la pamoja kwamba juhudi za nchi hizo tatu ndizo jitihada pekee za kimataifa zilizoleta matumaini ya kupatikana suluhisho la mgogoro wa Syria.
Tamko hilo limesema, kikao kijacho cha kimataifa kuhusu Syria kitafanyika sambamba na kikao cha pili cha kujadili njia za kuachiliwa huru watu waliotekwa nyara na walioko kizuizini, kukabidhiana miili ya watu waliouawa na kutambuliwa watu waliopotea. Kikao hicho kinatarajiwa kufanyika mwezi ujao wa Mei 2018 huko Astana, mji mkuu wa Kazakhstan.