Kuna uwezekano wa Trump kufikishwa mahakamani ili kusailiwa
https://parstoday.ir/sw/news/world-i43932-kuna_uwezekano_wa_trump_kufikishwa_mahakamani_ili_kusailiwa
Gazeti la Washington Post linalochapishwa nchini Marekani limeandika kuwa kuna uwezekano rais wa nchi hiyo Donald Trump akatakiwa afike mahakamani ili kusailiwa kuhusiana na kadhia ya kuingilia Russia mchakato wa uchaguzi wa rais wa Marekani wa mwaka 2016.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
May 02, 2018 03:14 UTC
  • Kuna uwezekano wa Trump kufikishwa mahakamani ili kusailiwa

Gazeti la Washington Post linalochapishwa nchini Marekani limeandika kuwa kuna uwezekano rais wa nchi hiyo Donald Trump akatakiwa afike mahakamani ili kusailiwa kuhusiana na kadhia ya kuingilia Russia mchakato wa uchaguzi wa rais wa Marekani wa mwaka 2016.

Kwa mujibu wa toleo la jana la gazeti hilo, Mchunguzi Maalumu wa faili la tuhuma za kuingilia Russia uchaguzi wa rais wa Marekani, Robert Mueller aliwaeleza mawakili wa Trump alipokutana nao mwishoni mwa mwezi Machi mwaka huu kwamba endapo rais huyo wa Marekani atakataa kuzungumza na wachunguzi wa faili hilo anaweza kutakiwa afike mahakamani.

Washington Post limefafanua kuwa Mueller alitoa indhari hiyo baada ya timu hiyo ya mawakili wa Trump kutamka kuwa rais huyo wa Marekani halazimiki kuzungumza na maafisa wanaohusika na uchunguzi wa kadhia hiyo.

Gazeti hilo limeongeza kuwa baada ya kikao hicho cha mwezi Machi, jopo la uchunguzi linaloongozwa na Robert Mueller lilikubali kuwapatia mawakili wa Trump maelezo zaidi ya nukta za masuali ambayo wachunguzi hao wangetaka kumuuliza kiongozi huyo.

Robert Mueller, Mchunguzi Maalum wa faili la uingiliaji wa Russia katika uchaguzi wa Marekani

Baada ya kupatiwa maelezo hayo, timu hiyo ya mawakili ilipanga jumla ya masuali 49 ambayo ilihisi Trump anaweza kutakiwa ayatolee majibu.

Kuingilia Russia uchaguzi wa mwaka 2016 wa rais wa Marekani ni moja ya masuala yaliyozusha makelele mengi wakati wa kampeni za uchaguzi huo, kati ya Trump na aliyekuwa mgombea urais kwa tiketi ya chama cha Democrat Hillary Clinton na hata baada ya uchaguzi huo.

Russia inatuhumiwa na vyombo vya usalama vya Marekani pamoja na chama cha Democrat kwamba iliingilia uchaguzi huo kwa lengo la kumsaidia Trump ashinde, tuhuma ambazo serikali ya Moscow imezikanusha.../