Yukiya Amano: Iran imefungamana kikamilifu na makubaliano ya nyuklia
https://parstoday.ir/sw/news/world-i44258-yukiya_amano_iran_imefungamana_kikamilifu_na_makubaliano_ya_nyuklia
Mkurugenzi Mkuu wa Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki (IAEA) kwa mara nyingine tena amethibitisha kwamba, Iran imeheshimu na kufungamana kikamilifu na makubaliano ya nyuklia yanayojulikana kama Mpango Kamili wa Pamoja wa Utekelezaji (JCPOA).
(last modified 2026-03-03T12:46:59+00:00 )
May 09, 2018 09:40 UTC
  • Yukiya Amano: Iran imefungamana kikamilifu na makubaliano ya nyuklia

Mkurugenzi Mkuu wa Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki (IAEA) kwa mara nyingine tena amethibitisha kwamba, Iran imeheshimu na kufungamana kikamilifu na makubaliano ya nyuklia yanayojulikana kama Mpango Kamili wa Pamoja wa Utekelezaji (JCPOA).

Yukiya Amano amesema hayo katika taarifa yake maalumu ambapo bila ya kuashiria hatua ya Rais Donald Trump wa Marekani ya kutangaza kuitoa nchi yake katika makubaliano hayo amesisitiza kuwa, Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomikia (IAEA) unafuatilia kwa karibu matukio yanayohusiana na makubaliano ya JCPOA na kwamba, kwa mujibu wa takwa la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa na idhini ya Bodi ya Magavana ya IAEA ya mwaka 2015 umekuwa ukisimamia suala la Iran kutekeleza au kutotekeleza majukumu yake kwa mujibu wa makubaliano hayo ya nyuklia.

Makao makuu ya Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki (IAEA)

Mkurugenzi Mkuu wa Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki (IAEA) ameongeza kuwa, taasisi hiyo inathibitisha kwamba, hadi sasa Iran imetekeleza ahadi na majukumu yake kwa mujibu wa makubaliano hayo yaliyoanza kutekelezwa Januari 2016.

Hii si mara ya kwanza kwa Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki kutangaza kwamba, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imefungamana kikamilifu na makubaliano hayo ya nyuklia.

Zaidi ya ripoti kumi zilizotolewa na Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki (IAEA) zimesema bayana kwamba, hakuna ushahidi wowote unaoonyesha kuwa, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imekengeuka makubaliano hayo.