Inspekta Mkuu wa IAEA ajiuzulu baada ya Marekani kujiondoa JCPOA
Inspekta Mkuu wa Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki IAEA ametangaza kujiuzulu ghafla, siku chache baada ya Rais Donald Trump kuiondoa Marekani kwenye makubaliano ya nyuklia ya Iran.
Msemaji wa IAEA amesema Inspekta Mkuu wa wakala huo, Tero Varjoranta, mwenye umri wa miaka 61 ametangaza kujiuzulu ghafla jana Ijumaa pasina kutoa maelezo ya kina juu ya hatua yake hiyo ya kushtukiza.
Varjoranta amekuwa Naibu Mkurugenzi Mkuu wa IAEA tangu mwaka 2013, na alikuwa akisimamia kitengo cha wakala huo chenye jukumu la kuhakikisha kuwa nchi wanachama zinafungamana na Mkataba wa Kuzuia Usambazwaji Silaha za Nyuklia (NPT).
Afisa huyo wa ngazi za juu wa IAEA ametangaza kujiuzulu siku tatu tu baada ya Rais Donald Trump wa Marekani kuchukua uamuzi wa upande mmoja wa kuiondoa nchi yake katika mapatano ya nyuklia ya Iran ya JCPOA.

Hatua hiyo ya Marekani imepingwa na nchi zingine tanzu zilizofikia mapatano hayo ambazo ni China, Russia, Uingereza, Ufaransa na Ujerumani, ambazo zimetoa taarifa zikisisitiza kufungamana na mapatano hayo ya kimataifa.
Mkurugenzi Mkuu wa IAEA, Yukiya Amano amemteua Massimo Aparo kukaimu nafasi hiyo iliyoachwa wazi na Tero Varjoranta raia wa Finland.