Korea Kaskazini yatishia kufuta mkutano wake na Marekani
Korea Kaskazini imetishia kufuta mkutano kati ya kiongozi wake, Kim Jong-un na Rais Donald Trump wa Marekani, kutokana na kile inachodai kuwa ni chokochoko za Washington na Korea Kusini dhidi yake.
Hii ni baada ya Marekani na Korea Kusini kufanya maneva makubwa ya vikosi vyao vya anga katika Peninsula ya Korea kwa kisingizio cha kuimarisha uwezo wa kushambulia na kujihami wa nchi hizo mbili.
Shirika la habari la serikali ya Korea Kaskazini KCNA limetangaza kuwa, "Mazoezi haya ya kijeshi dhidi yetu yanayofanyika Korea Kusini ni kinyume kabisa na Tangazo la Panmunjom, na ni uchokozi wa makusudi ulio dhidi ya hatua chanya zilizofikiwa katika Peninsula ya Korea."
Wakati huo huo, Korea Kaskazini imesimamisha kwa muda usiojulikana mkutano wa ngazi ya juu uliotazamiwa kufanyika leo Jumatano kati yake na Korea Kusini.
Mapema mwezi huu, Pyongyang kadhalika ilikosoa vikali kile ilichokitaja kama upotoshaji wa makusudi wa Washington, kwamba sera za Trump za kushadidisha vikwazo na mashinikizo ya kisiasa dhidi ya nchi hiyo ndizo zilizopelekea Korea Kaskazini kukubali kuketi kwenye meza ya mazungumzo.
Kwa mujibu wa Pyongyang, uamuzi wa kukutana na Trump na pia kusimamisha majaribio ya silaha za nyuklia na makombora ya balestiki umefikiwa na kiongozi wa Korea Kaskazini mwenyewe, na wala sio kutokana na mashinikizo na vikwazo.
Kim Jong-un anatazamiwa kukutana na Rais Donald Trump wa Marekani mwezi ujao wa Juni nchini Singapore.