Onyo la Korea Kaskazini kwa Marekani, lailazimisha Washington kurejea nyuma
Kufuatia onyo kali la Korea Kaskazini la kutaka kuvunja kikao tarajiwa kati ya kiongozi wa nchi hiyo na Rais wa Marekani hapo tarehe 12 Juni mwaka huu, hatimaye Washington imelazimika kutangaza kwamba ndege za kivita zenye kubeba mabomu ya nyuklia hazitashirki katika maneva ya pamoja ya anga ya nchi hiyo na Korea Kusini.
Mazungumzo kati ya Kim Jong-un, Kiongozi wa Korea Kaskazini na Rais Donald Trump wa Marekani yamepangwa kufanyika tarehe 12 Juni nchini Singapore. Jumanne iliyopita Korea Kaskazini na katika radiamali yake dhidi ya maneva ya pamoja ya majeshi ya anga ya Marekani na Korea Kusini, ilitangaza kwamba huwenda kiongozi wa nchi hiyo akavunja ratiba yake ya kukutana na rais wa Marekani.
Kadhalika katika kulalamikia maneva hayo, Pyongyang ilifuta kikao cha viongozi wa ngazi ya mawaziri kati ya nchi yake na Korea Kusini. Kufuatia misimamo hiyo ya Korea Kaskazini hatimaye Washington imelazimika kurejea nyuma na kutangaza wazi kwamba ndege za kivita zenye kubeba mabomu ya nyuklia hazitashiriki katika maneva ya pamoja ya anga yanayoshirikisha Marekani na Korea Kusini. Maneva ya pamoja ya anga ya nchi mbili hizo yalianza tarehe 11 mwezi huu na yanatazamiwa kumalizika tarehe 25 katika Rasi ya Korea. Hii ni katika hali ambayo siku chache zilizopita kiongozi wa Korea Kaskazini alitangaza kusimamisha majaribio yote ya silaha za nyuklia na makombora ya balestiki ya nchi hiyo.
Aidha kiongozi huyo aliwaachilia huru raia watatu wa Marekani waliokuwa wanashikiliwa katika jela za Korea Kaskazini kwa tuhuma za kufanya ujasusi na hatua za kiuhasama dhidi ya Pyongyang. Raia hao walitolewa jela wiki iliyopita na kurejea Washington pamoja na Mike Pompeo, Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani. Pyongyang ilitangaza kwamba, imewaachilia huru Wamarekani hao kwa madhumuni ya kuonyesha nia njema.