Joto ambalo halijawahi kushuhudiwa Pakistan laendelea kusababisha maafa
Hadi sasa ongezeko la joto kali ambalo halijawahi kushuhudiwa mjini Karachi, Pakistan limesababisha maafa ya makumi ya watu.
Taasisi binafsi ya Edhi Foundation ya nchi hiyo sambamba na kuashiria hali ya hewa mjini Karachi na ongezeko la nyuzijoto iliyopindukia 42, imesema kuwa imeendelea kuokota miili ya watu waliopoteza maisha kutokana na janga hilo la kimaumbile. Kwa mujibu wa taasisi hiyo, hadi sasa makumi ya raia wa nchi hiyo wamepoteza maisha suala ambalo linatia wasi wasi mkubwa.
Aidha shirika hilo ambalo lina wadhifa wa kusimamia miradi kadhaa ya afya nchini Pakistan limesema kuwa, katika kipindi cha siku nne zilizopita hadi sasa limepokea miili ya watu 180 idadi ambayo ni mara mbili zaidi ya vifo ambavyo huwa vinatokea kwa sababu ya joto kali katika miaka mingine. Limeongeza kwamba akthari ya wahanga wa maafa hayo wanatokana na kuzidiwa na joto kali. Ongezeko la joto kali nchini Pakistan limepanda tangu mwanzoni mwa mwezi mtukufu wa Ramadhani. Hivi karibuni pia iliarifiwa kuwa watu wasiopungua 65 walipoteza maisha kutokana na joto kali mjini Karachi.
Hii ni katika hali ambayo mamlaka ya hali ya hewa nchini humo imetahadharisha juu ya uwezekano wa kushtadi zaidi kiwango cha joto katika siku mbili au tatu zijazo. Kwa mujibu wa taasisi hiyo katika siku hizo kiwango cha joto kinatazamiwa kufikia nyuzijoto 44. Inaelezwa kuwa mwezi Juni 2015 karibu watu 1200 walipoteza maisha kutokana na joto kali kusini mwa nchi hiyo. Theluthi mbili ya wahanga hao ilihusiana na watu wasiokuwa na makazi.