Ujerumani yaipigia magoti Iran, yaitaka isijiondoe JCPOA
Waziri wa Mambo ya Nje wa Ujerumani amesema Berlin iko tayari kuimarisha uhusiano wa kiuchumi na Jamhuri ya Kiislamu ya Iran madhali Tehran itaendelea kufungamana na mapatano ya nyuklia ya JCPOA.
Heiko Maas, aliyasema hayo jana Jumanne akihutubu katika mkutano wa Global Solutions Summit mjini Berlin na kufafanua kuwa, "Tutaendelea kufanya jitihada za kutimiza azma ya Iran ya kuhuisha uchumi wake na kuimarisha uhusiano wa kibiashara, madhali Tehran haitajitoa kwenye makubaliano ya JCPOA.
Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imekuwa ikisisitiza kuwa, kubakia au kuondoka kwake kwenye mapatano hayo ya kimataifa, kutategemea dhamana madhubuti itakayotolewa na Umoja wa Ulaya.
Hii ni katika hali ambayo, Mkuu wa Sera za Kigeni wa Umoja wa Ulaya, Federica Mogherini alisema siku ya Jumapili baada ya kumalizika kikao cha mawaziri wa mambo ya nje wa Umoja wa Ulaya mjini Brussels, Ubelgiji kuwa, umoja huo hivi sasa unajadili njia za kuipa Iran vivutio vya kiuchumi ili kuyalinda mapatano hayo.
Alisisitiza kuwa, kulindwa JCPOA hakuna manufaa ya kiuchumi tu kwa Umoja wa Ulaya, bali umoja huo unayahitajia mapatano hayo katika masuala yake ya kiusalama.
Itakumbukwa kuwa tarehe 8 mwezi huu, Rais wa Marekani, Donald Trump alitangaza kuitoa nchi yake kwenye mapatano ya JCPOA licha ya kwamba Washington ilikuwa mstari wa mbele kuyafanikisha wakati wa urais wa Barack Obama.