Waziri wa Mambo ya Nje wa Ujerumani: Marekani haiaminiki tena
Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Ujerumani amejibu matamshi na hujuma ya maneno ya Rais wa Marekani aliyeutaja Umoja wa Ulaya kuwa ni "adui" kwa kusema: Ulaya haiwezi tena kuitegemea Ikulu ya Rais wa Marekani.
Heiko Maas amesema kuwa, Ulaya haipaswi kugawanyika kutokana na mashambulizi makali ya maneno na ujumbe zisizo na maana za Donald Trump kwenye mtandao wa kijamii wa Twitter.
Trump ambaye amewaudhi washirika wa Ulaya wa Marekani kwa kuzidisha shuru wa forodha kwa bidhaa za nchi za Ulaya zinazopelekwa Marekani, Jumapili iliyopita aliiambia televisheni ya CBS kwamba Umoja wa Ulaya na China ni maadui wakubwa zaidi wa Marekani.
Vilevile aliishambulia Ujerumani kutokana na kununua mafuta na gesi kutoka Russia na kusema imekuwa mateka wa Moscow.

Rais wa Marekani pia amekosoa serikali ya Kansela wa Ujerumani, Angela Merkel kutokana na siasa zake za milango wazi na kuwakaribisha wahajiri na wakimbizi.