Mike Pompeo: Vikwazo vya Marekani dhidi ya Korea Kaskazini vitaendelea
https://parstoday.ir/sw/news/world-i46873-mike_pompeo_vikwazo_vya_marekani_dhidi_ya_korea_kaskazini_vitaendelea
Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani amesema kuwa kufikiwa makubaliano kamili ya nyuklia kati ya nchi yake na Korea Kaskazini, kutategemea muda mrefu na kwamba katika kipindi hicho vikwazo vya Washington dhidi ya Pyongyang vitaendelea kuwepo.
(last modified 2023-11-27T12:14:11+00:00 )
Jul 19, 2018 07:24 UTC
  • Mike Pompeo: Vikwazo vya Marekani dhidi ya Korea Kaskazini vitaendelea

Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani amesema kuwa kufikiwa makubaliano kamili ya nyuklia kati ya nchi yake na Korea Kaskazini, kutategemea muda mrefu na kwamba katika kipindi hicho vikwazo vya Washington dhidi ya Pyongyang vitaendelea kuwepo.

Mike Pompeo ameyasema hayo katika kikao cha baraza la serikali ya Marekani wakati akiwasilisha ripoti kuhusiana na mazungumzo yake aliyoyafanya hivi karibuni na viongozi wa Korea Kaskazini na kusema kuwa, hatua nyingi zimechukuliwa ambapo baadhi zinahitajia muda zaidi, lakini akasisitiza kwamba, hatua zote hizo zinachukuliwa katika anga ya mwendelezo wa vikwazo. Kadhalika Pompeo amezungumzia kuanza kuwasili mabaki ya miili ya askari wa Marekani kutoka Korea Kaskazini na kusema kuwa, miili ya kwanza ya askari hao itaanza kuwasili katika kipindi cha wiki mbilizi zijazo na kwamba suala hilo ni muhimu sana kwa familia za askari hao.

Mike Pompeo, Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani alipowasili Pyongyang hivi karibuni

Matamshi ya Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani kwamba viwazo vya Marekani vitaendelea dhidi ya Pyongyang yametolewa ikiwa ni baada ya serikali ya Korea Kaskazini kukubali kuikabidhi Washington, mabaki ya miili ya askari 55 wa Kimarekani ambao waliuawa katika vita vya Korea mbili kati ya mwaka 1950 hadi 1953. Licha ya Marekani kusisitizia juu ya udharura wa kuendelezwa vikwazo dhidi ya Korea Kaskazini, lakini Alexander Matsegora, balozi wa Russia mjini Pyongyang amenukuliwa akisema kuwa, ni lazima vikwazo dhidi ya nchi hiyo vipunguzwe kupitia ushirikiano wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa. Hivi karibuni Mike Pompeo alizitembelea nchi za Vietnam, Imarati, Mexico na Korea Kaskazini.