Russia: Kuna uwekezano Marekani ikaishambulia kijeshi Venezuela
Balozi wa Russia nchini Venezuela ameonyesha masikitiko yake kutokana na uwezekano wa Marekani kuchukua hatua ya kijeshi dhidi ya nchi hiyo.
Vladimir Zamsky, ameyasema hayo katika mahojiano na Shirika la Habari la Sputnik na kuongeza kuwa, kwa kuzingatia tajriba ya utendajikazi wake, Marekani imeendelea kusisitiza machaguo kadhaa, likiwemo chaguo la kijeshi dhidi ya Venezuela. Mwanadiplomasia huyo wa Russia amebainisha kwamba, suala hilo ni hatari kubwa hususan kwamba Marekani imekuwa ikizungumzia stratijia ambayo inasisitiza kuyaacha wazi maeneo yote ya kusini mwa Marekani. Hayo yanajiri katika hali ambayo hivi karibuni Rais Nicolás Maduro wa Venezuela alilitaka jeshi la nchi hiyo kujiweka tayari kwa ajili ya kukabiliana na hujuma tarajiwa za Marekani dhidi ya nchi hiyo.
Maduro alitoa indhari hiyo kwa jeshi la nchi yake kufuatia habari na ripoti zilizotolewa nchini Marekani kwamba, mwaka jana wa 2017 Rais Donald Trump wa nchi hiyo alikuwa na mpango wa kutaka kuishambulia kijeshi Venezuela. Tarehe 11 Agosti mwaka jana Rais Donald Trump wa Marekani akizungumza na waandishi wa habari katika jimbo la New Jersey, alinukuliwa akisema kuwa kuna uwezekano wa Marekani kuishambulia kijeshi Venezuela, matamshi ambayo yaliwakasirisha mno viongozi wa Caracas.