Marekani imewakabidhi silaha magaidi Syria
Tovuti moja ya habari imefichua kuwa Marekani hadi sasa imeshatoa msaada wa tani elfu tatu za silaha kwa magaidi wa Al Qaeda na washirika wao nchini Syria.
Katika ropoti hiyo ambayo ni muendelezo wa kufichuliwa habari za msaada wa Marekani kwa makundi ya kigaidi, tovuti ya moonofalabama.org imefichua, ‘Marekani, kupitia shirika lake la kijasusi la CIA, inaendelea kutoa msaada wa maelfu ya tani za silaha kwa Al Qaeda na makundi mengine ya kigaidi Syria.”
Ripoti hiyo imedokeza kuwa, silaha hizo zimekuwa zikiwafikia magaidi hasa wa mtandao wa Al Qaeda nchini Syria kupitia bandari ya Aqaba ya nchini Jordan. Aghalabu ya silaha hizo zimetengenezwa na mashirika ya eneo la Mashariki mwa Ulaya. Ripoti hiyo imetoa mfano na kusema tarehe tatu Novemba mwaka 2015, kontena za silaha na mabomu ziliwasili katika Bandari ya Aqaba kutoka Bulgaria kwa ajili ya kutumwa kwa magaidi walioko nchini Syria. Kati ya silaha zilizonunuliwa na Marekani kwa ajili ya magaidi wa Syria ni pamoja na bunduki, mabomu ya kupigia vifaru na makombora ya masafa mafupi. Aidha ripoti hiyo imefichua kuwa tarehe tatu Disemba tani elfu moja za silaha kutoka Romania ziliingia Uturuki na kufikishiwa magaidi nchini Syria.
Kwa muda mrefu sasa serikali ya Syria imekuwa ikisisitiza kuwa magaidi nchini humo wanapata misaada ya kifedha na kisilaha kutoka kwa nchi za Magharibi hasa Marekani na waitifaki wake katika eneo hili ambao ni Saudi Arabia, Qatar, Uturuki na utawala haramu wa Israel. Karibu watu nusu milioni wameshapoteza maisha tokea magaidi waanzishe kampeni ya kumuondoa madarakani Rais Bashar al Assad wa Syria mwaka 2011.