Imran Khan aapishwa kama waziri mkuu mpya wa Pakistan
Nyota wa zamani wa mchezo wa cricket nchini Pakistan amechukua nafasi ya waziri mkuu mpya wa nchi hiyo kufuatia idhini ya bunge.
Khan, mwenye umri wa miaka 65, ameapishwa leo kama Waziri Mkuu wa 22 wa Pakistan katika sherehe iliyohudhuriwa na viongozi kadhaa na wachezaji wa cricket mjini Islamabad.
Chama cha Khan cha Pakistan Tehreek-e-Insaf (PTI) kilishinda uchaguzi wa bunge uliofanyika Julai lakini hakikuweza kupata ushindi mutlaki wa kuunda serikali na kwa msingi huo inatazamiwa kuwa ataunda serikali ya mseto.
Katika ucahguzi uliofanyika bungeni jana, Khan alipata kura 176 huku mpinzani wake wa karibu Shehbaz Sharif wa chama cha Pakistan Muslim League-Nawaz (PML-N) akipata kura 96 tu.
Wapinzani wanadai kuwa uchaguzi wa bunge wa Julai 25 ulikumbwa na wizi wa kura uliotekelezwa na jeshi la nchi hiyo ambalo limewahi kutawala nchi hiyo kwa miongo kadhaa. Hata hivyo jeshi limepinga tuhuma hizo.