Russia: Iran iko kihalali nchini Syria na sisi tunaliheshimu hilo
(last modified Sat, 25 Aug 2018 02:20:59 GMT )
Aug 25, 2018 02:20 UTC
  • Russia: Iran iko kihalali nchini Syria na sisi tunaliheshimu hilo

Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Russia, Sergei Ryabkov amesema kuwa nchi yake inaheshimu uwepo wa Iran nchini Syria kwani iko huko kihalali na kwa mwaliko wa serikali halali ya nchi hiyo.

Shirika la habari la Tass limeripoti habari hiyo na kumnukuu Ryabkov akisema kuwa, Iran iko nchini Syria kwa mwaliko rasmi wa serikali ya nchi hiyo ambayo imeiomba Tehran iisaidie kupambana na magaidi.

Tunaheshimu sana hatua za Iran za kulinnda usalama wake ikiwa ni pamoja na kuweko kwake nchini Syria kutokana na mwaliko wa serikali halali ya nchi hiyo. 

Matamshi hayo ya Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Russia yametolewa baada ya kuonana na ujumbe wa Marekani mjini Geneva, Uswisi na kujadiliana kadhia ya Syria.

Marais wa Marekani na Russia

 

Amesema, Russia ina mambo mengi isiyokubaliana na Marekani kuhusu suala la Syria hata hivyo amesema, Moscow iko tayari kuzungumzia na Washington kuhusu hali ya mambo katika nchi hiyo. 

Vile vile amesema, Russia inashirikiana na Iran katika kadhia ya Syria chini ya msingi wa mazungumzo ya Astana na kuongeza kuwa, karibuni hivi kutafanyika mawasiliano mapya kuhusu suala hilo ikiwa ni pamoja na kuzingatia pia mazungumzo ya Geneva.

Wakati huo huo Naibu huyo wa Waziri wa Mambo ya Nje wa Russia amesema, nchi yake imeweka mezani machaguo yote ya kukabiliana na vikwazo vipya vya Marekani dhidi yake.

Sergei Ryabkov alisisitiza hayo jana Ijumaa na kuongeza kuwa, hadi hivi sasa Kremlin haijaona ishara zozote kutoka kwa Marekani za kutaka kuwa na uhusiano wa kawaida na Moscow.