Wanawake Waislamu Quebec, Canada kupigwa marufuku kuvaa Hijabu
Serikali ya Waziri Mkuu mteule wa jimbo la Quebec nchini Canada imeazimia kuwapiga marufuku wanawake Waislamu wa eneo hilo kuvaa hijabu ya aina yeyote ikiwemo mitandio ya kichwani.
Kwa mujibu wa tovuti ya habari ya Middle East Eye, Francois Legault Waziri Mkuu mteule wa Quebec ambaye chama chake cha mrengo wa kulia kimeshinda katika uchaguzi wa hivi karibuni ameahidi kuwasilisha muswada wa sheria itakayowapiga marufuku walimu, maafisa wa polisi, majaji pamoja na wafanyakazi wengine wa sekta za umma kuvaa vazi lenye 'nembo ya kidini'.
Baraza Kuu la Wanawake Waislamu Canada limesema sheria hiyo inawalenga wanawake Waislamu katika jimbo la Quebec kwa njia isiyo ya moja kwa moja.
Mwezi Oktoba mwaka jana, bunge la kieneo la Quebec lilipiga kura 65-51 kuunga mkono sheria ya kuwapiga marufuku wanawake Waislamu kuvaa Hijabu yenye kufunika uso mzima maarufu kama niqab wakiwa wanatumia huduma za umma.
Pamoja na kuwa sheria hiyo haikutaja vazi maalumu, lakini wengi waliitafsiri kuwa ni yenye kuwazuia wanawake Waislamu kuvaa niqab au burqa ambazo ni kati ya Hijabu zinazotumiwa na baadhi ya wanawake.
Hii haitakuwa mara ya kwanza kwa wanawake Waislamu kupigwa marufuku kuvaa aina mbali mbali za Hijabu katika nchi za Magharibi.
Hii ni katika hali ambayo, huko nyuma, Justin Trudeau, Waziri Mkuu wa Canada sanjari na kuunga mkono uhuru wa mtu binafsi na haki ya chaguo la wanawake wa Kiislamu alisema kuwa, urafiki na maelewano kwa raia wa nchi hiyo ni jambo lenye kupewa umuhimu.