Kufeli vibaya Marekani nchini Afghanistan
https://parstoday.ir/sw/news/world-i48671-kufeli_vibaya_marekani_nchini_afghanistan
Sambamba na kumbukumbu ya miaka 17 ya kuvamiwa Afghanistan na Marekani, uchunguzi wa maoni unaonesha kuwa wananchi wengi wa Afghanistan wanaamini kwamba Marekani imeshindwa na kufeli vibaya nchini humo.
(last modified 2026-01-14T08:12:18+00:00 )
Oct 09, 2018 02:21 UTC
  • Kufeli vibaya Marekani nchini Afghanistan

Sambamba na kumbukumbu ya miaka 17 ya kuvamiwa Afghanistan na Marekani, uchunguzi wa maoni unaonesha kuwa wananchi wengi wa Afghanistan wanaamini kwamba Marekani imeshindwa na kufeli vibaya nchini humo.

Kwa mujibu wa uchunguzi huo wa maoni uliofanywa na taasisi ya Pew yenye makao yake mjini Washington, Marekani, sehemu kubwa ya walioshiriki kwenye maoni hayo wamesema kuwa Marekani imeshindwa kijeshi huko Afghanistan na wanataka wanajeshi wa nchi hiyo waondoke nchini humo. Hata takwimu na ripoti mbalimbali zinazotolewa kuhusu utendaji wa wanajeshi wa Marekani na NATO huko Afghanistan unaonesha kuwa Washington umefeli vibaya. Mwaka 2001, Marekani ilituma wanajeshi wake kwenda kuivamia Afghanistan kwa madai ya kupambana na ugaidi, kuleta amani ya kudumu na kuwaandalia mazingira na maisha bora wananchi wa Afghanistan. Hata hivyo matunda pekee yaliyopatikana kutokana na kukaliwa kwa mabavu Afghanistan na majeshi vamizi ya Marekani ni ongezeko kubwa la mauaji ya raia kiasi kwamba katika kipindi cha miezi 9 iliyopita, Umoja wa Mataifa umeripoti kuongezeka mara 46 mauaji ya raia katika mashambulizi ya kigaidi ikilinganishwa na miaka iliyopita. Balaa jingine lililosababishwa na uvamizi wa Marekani huko Afghanistan ni kuongezeka uzalishaji wa madawa ya kulevya na magendo ya mihadarati pamoja na athari mbaya za kiroho na kisaikolojia wanazopata raia wa nchi hiyo kutokana na kukaliwa kwa mabavu nchi yao. Hiyo ni sehemu ndogo tu ya madhara mengi yaliyosababishwa na uvamizi wa kijeshi wa Marekani huko Afghanistan. 

Ukulima wa mmea wa mpopi unaozalisha madawa ya kulevya umeongezeka sana nchini Afghanistan baada ya Marekani kuivamia nchi hiyo

Nukta nyingine ya kuzingatia hapa ni kwamba, Marekani inadai kuwa iliivamia kijeshi Afghanistan kwa shabaha ya kuwaokoa wananchi wa nchi hiyo lakini hivi sasa Washington ndiye msababishaji mkubwa wa ukosefu wa amani na kuongezeka vitendo vya kigaidi huko Afghanistan kiasi kwamba taasisi moja isiyo ya kiserikali inayoijulikana kwa jina la "Kundi la Kupigania Usalama wa Raia Afghanistan" imesema katika ripoti yake ya hivi karibuni kabisa kuwa,  zaidi ya raia mia moja wameuliwa kwenye mashambulizi ya anga ya Marekani na NATO katika mikoa 12 ya Afghanistan kwenye kipindi cha mwezi Septemba 2018 pekee.

"Nadhari" ni mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Kabul. Anasema: Uwepo wa wanajeshi wa Marekani nchini Afghanistan ndiyo sababu kuu ya kuongezeka ukosefu wa amani na utulivu na vitendo vya magenge ya kigaidi nchini humo. Marekani ina malengo yaliyo zaidi na kuwepo kwake kijeshi nchini Afghanistan na ndio maana haitaki kabisa kupatikana amani ya kweli nchini humo.

Ijapokuwa Afghanistan ni nchi maskini na imekumbwa na mapigano ya ndani kwa makumi ya miaka sasa, lakini ina umuhimu mkubwa kijiografia na ina utajiri mkubwa wa madini ambao haujaguswa. Inatathminiwa kuwa utajiri wa madini wa Afghanistan una thamani ya dola bilioni elfu tatu. Ni kwa sababu hiyo ndio maana muda wote Marekani ilikuwa inasubiri fursa ndogo tu ya kuivamia na kuipora Afghanistan utajiri wake wa maliasili. Mashambulizi yenye utata ya Septemba 11 huko Marekani yalimpa fursa George Bush, rais wa wakati huo wa Marekani kuivamia kijeshi Afghanistan na kutimiza ndoto ya siku nyingi ya Washinigton.

Mauaji ya raia limekuwa ni jambo la kila siku nchini Afghanistan

 

Michael Hughes, mtaalamu wa masuala ya kisiasa anasema: Mkakati wa Marekani huko Afghanistan ni kuelekea kwenye masuala ya biashara. Juhudi za Marekani zinalenga kubakia kwa miaka mingi Afghanistan kupitia madai ya kuchimba madini. Jambo hilo linatumiwa na mrengo wa kulia wa chama cha Republican huko Marekani kuficha kufeli kwao nchini Afghanistan.

Alaakullihaal, miaka 17 ya kukaliwa kimabavu Afghanistan na Marekani na sisitizo la majenerali wa kijeshi wa nchi hiyo la kuendelea kuweko nchini humo ni mambo yanayobainisha ukweli mchungu kwa wananchi wa Afghanistan kwamba inachofikiria Marekani ni kujinufaisha binafsi tu na haiwafikirii kabisa wananchi wa nchi hiyo. Hatari kubwa zaidi ni kwamba Marekani hivi sasa imebadilisha muundo wake wa kuikalia kwa mabavu Afghanistan na imekuja na stratijia ya kibiashara na kuchimba madini, hii ikiwa na maana ya kutoa nafasi kwa mashirika yake ya mauaji kama vile Black Water kujizaititi zaidi huko Afghanistan kwa madai yakulinda usalama bila ya kujali utamaduni, ada, desturi na muundo wa kidini wa wananchi hao Waislamu.