Taliban wanawakata vidole watu waliopiga kura katika uchaguzi wa Bunge
Kundi la Taliban nchin Afghanistan linawasaka na kuwakata vidole raia walioshiriki katika zoezi la uchaguzi wa Bunge nchini humo.
Habari zinasema kuwa, wanachama wa kundi la Taliban wanawakamata raia ambao vidole vyao vina rangi iliyotumika katika zoezi la kupiga kura na kukata vidole vyao.
Shah Mahmoud Naimi ambaye ni mjumbe wa Baraza la Mkoa wa Farah nchini Afghanistan amesema kuwa, kundi la Taliban limewakata vidole wapiga kura wasiopungua 10 katika eneo hilo.
Naimi ameongeza kuwa, kundi hilo pia limewateka nyara raia kadhaa kwa sababu ya kushiriki katika zoezi la kupiga kura.
Wanaharakati wa kutetea haki za kiraia katika mkoa wa Farah pia wamesema wapiganaji wa kundi hilo wameua wapigaji kura watano katika eneo hilo.
Uchaguzi wa Bunge la Taifa la Afghanistan ulifanyika katika siku za tarehe 20 na 21 mwezi huu katika mikoa 32 kati ya 34 ya Afghanistan. Zoezi hilo lilisimamishwa katika mikoa ya Qandahar na Ghazni kutokana na ukosefu wa usalama na mashambulizi ya wapiganaji wa kundi la Taliban.
Kundi hilo lilitangaza rasmi kuwa litafanya kila liwezekanalo kuhakikisha kuwa uchaguzi huo haufanyiki. Makumi ya watu wameripotiwa kuuawa katika miripuko iliyotokea katika maeneo mbalimbali ya Afghanistan na makumi ya wengine wamejeruhiwa kabla na wakati wa kufanyika zoezi hilo.