Umoja wa Mataifa: Wanahabari 88 wameuawa mwaka huu 2018
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa amesema jumla ya waandishi wa habari na wafanyakazi wengine katika sekta ya upashanaji habari 85 wameuawa tokea mwanzoni mwa mwaka huu 2018 hadi sasa katika sehemu mbalimbali duniani.
Antonio Guterres ameyasema hayo kwa mnasaba wa Siku ya Kimataifa ya Kupambana na Jinai dhidi ya Waandishi wa Habari inayoadhimishwa hii leo kote duniani. Amesema kuhujumiwa waandishi wa habari hakupaswi kufumbiwa macho, na kwamba jamii zinapaswa kujiandaa kulipa gharama za kutochukuliwa hatua za kisheria wanaowashambulia wanahabari.
Ripoti hiyo ya UN imetolewa wakati huu ambapo dunia inaendelea kulaani mauaji ya kikatili ya Jamal Khashoggi, mwandishi mashuhuri wa habari na mpinzani wa utawala wa Aal-Saud, katika ubalozi mdogo wa Saudia mjini Istanbul, Uturuki Oktoba Pili mwaka huu.
Kwa mujibu wa takwimu za UN, kati ya mwaka 2006 na 2017, wanahabari zaidi ya 1,000 waliuawa na wengine kutoweka katika mazingira ya kutatanisha kwa sababu ya kutoa taarifa kwa umma na kufichua kashfa mbalimbali.

Disemba mwaka jana 2017, Shirika la Maripota Wasio na Mipaka (RSF) lilisema jumla ya waandishi wa habari na wafanyakazi wengine katika sekta ya upashaji habari 65 waliuawa mwaka huo katika sehemu mbali mbali duniani.
Kwa mujibu wa Shirikisho la Kimataifa la Waandishi Habari (IFJ), wanahabari 93 waliuawa kwa makusudi au katika machafuko yaliyotokea kwenye maeneo mbalimbali ya dunia mwaka 2016.