EU: Makubaliano ya nyuklia ya Iran hayana chaguo jengine mbadala
Kamishna wa Umoja wa Ulaya wa Uadilifu, amesema hakuna chaguo jengine lolote mbadala na lenye itibari kwa ajili ya makubaliano ya nyuklia ya Iran, JCPOA.
Věra Jourová, Kamishna wa Umoja wa Ulaya wa Uadilifu, Wanunuzi na Usawa wa Jinsia amekieleza kikao cha mzunguko cha Bunge la Ulaya kwamba kulindwa makubaliano ya nyuklia ya Iran ni miongoni mwa maudhui muhimu kwa ajili ya usalama wa jamii ya kimataifa.
Afisa huyo wa EU ameongeza kuwa, taasisi hiyo haivitambui vikwazo vya nje ya mipaka vilivyowekwa na Marekani baada ya nchi hiyo kujitoa kwenye makubaliano ya JCPOA.
Bi Věra Jourová amesisitiza kuwa Umoja wa Ulaya hauwezi kukubali uamuliwe na Marekani kuhusu biashara halali kisheria ambayo umoja huo unafanya na nchi fulani.

Kamishna wa Umoja wa Ulaya wa Uadilifu, Wanunuzi na Usawa wa Jinsia amebainisha kuwa hatua endelevu zinaendelea kuchukuliwa kwa uongozi wa Ufaransa, Ujerumani na Uingereza kwa lengo la kuendelea kutekeleza kikamilifu na kwa uathirifu makubaliano ya nyuklia ya JCPOA katika pande zake zote na kulingana na azimio nambari 2231 la Baraza la Umoja wa Mataifa.
Licha ya hatua ya upande mmoja iliyochukuliwa na rais wa Marekani Donald Trump ya kujitoa kwenye makubaliano ya nyuklia yanayojulikana kama Mpango Kamili wa Pamoja wa Utekelezaji (JCPOA), nchi nyingine tano zilizosaini makubaliano hayo na Iran zimesisitiza kuwa zitaendelea kubaki kwenye JCPOA.../