Afghanistan katika hatari ya kutumbukia kwenye moto wa vita vya kimadhehebu
Mlipuko wa bomu uliotokea katika jimbo la Khost kusini mashariki mwa Afghanistan Ijumaa iliyopita ulipelekea karibu watu 30 kupoteza maisha na makumi ya wengine kujeruhiwa.
Mlipuko huo ulitokea adhuhuri na wakati wa Swala katika msikiti mmoja ulioko katika kambi ya jeshi. Kwa kuzingatia shambulio jingine la hivi karibuni la kigaidi katika sherehe ya Maulidi ya Mtume SAW katika hoteli ya Uranus mjini Kabul ambapo takribani maulama na hadhirina sitini waliuawa, tunaweza kusema kuwa, lengo la mashambulio ya kigaidi nchini humo ni kutaka kuitumbukia nchi hiyo katika vita vya kikaumu na kimadhehebu, jambo ambalo ni hatari mno kwa mustakabali wa amani na uthabiti wa Afghanistan.
Licha ya kuwa, nchi ya Afghanistan katika kipindi miongo minne iliyopita ima ilikuwa ikikabiliwa na vita vya wenyewe kwa wenyewe au vya wavamizi, lakini hakuna wakati ambao wananchi wa nchi hiyo wameshuhudia mashambulio ya kikaumu kkama hivi sasa; kwani huko nyuma madhehebu zote zilikuwa zikiishi pamoja na kwa amani bila ya mapigano wala vurugu baina yao au mizozo ya kikaumu.
Iqbal Bozorg mtaalamu wa masuala ya kisiasa anasema kuwa: Hakuna wakati ambao baina ya wananchi wa Afghanistan kulizungumziwa suala la ukaumu na madhehebu na hakuna wakati ambao suala hilo lilipelekea kuibuka vurugu na machafuko. Hivyo basi mashambulio dhidi ya sherehe na marasimu ya kidini ni tukio jipya nchini Afghanistan ambapo waungaji mkono wake wanafuatilia malengo machafu.
Hii ina maana kuwa, maadui wa wananchi wa Afghanistan wameamua kulenga umoja wa kimadhehebu na kitaifa wa nchi hiyo ili kwa njia hiyo waweze kuwagonganisha na kuwapambanisha wafuasi wa madhehebu mbalimbali na hivyo kuwatumbukiza katika vita vya kikaumu na kimadhehebu nchini humo. Bila kujali ni kikundi gani miongoni mwa makundi ya kigaidi ambayo yanapanga na kutekeleza mashambulio hayo, lakini kuendelea hali hiyo kunatufanya tuzingatie nukta kadhaa. Mosi ni kuwa, mashambulio ya kigaidi ya kimadhehebu nchini Afghanistan yanatokea katika maeneo kama ya Swala ya Ijumaa na hoteli ambayo yana ulinzi mkali. Kwa msingi huo, kutokea mashambulio kama hayo, kunaweza kutilia alama ya swali uwezo wa jeshi na kikosi cha polisi ya Afghanistan.
Nukta ya pili ni kuwa, kuendelea vita vya Taliban nchini Afghanistan kumepelekea pia kuongezeka machafuko ya umwagaji damu katika nchi hiyo. Kuibuka makundi yaliyojitenga na kundi hilo na kupinga mrengo wenye misimamo mikali suala la Taliban kujiunga na mwenendo wa amani, daima ni jambo ambalo limekuwa likipelekea kushadidi mashambulio ya kigaidi katika nchi hiyo. Nukta ya tatu ni hii kwamba, kuendelea mashambulio ya wanamgambo wa Taliban nchini Afghanistan kumepelea kushadidi pia harakati za makundi ya kigaidi nchini humo kama lile la Daesh.
Kwa kuzingatia kwamba, makundi mengi ya kigaidi nchini Afghanistan na Pakistan yana chimbuko la fikra za kundi potofu la Kiwahabi tunaweza kutabiri kwamba, makundi hayo ya kigaidi na yenye mrengo wa kikaumu yatashadidisha harakati zake nchini Afghanistan. Siegfried Wolf mtaalamu wa masuala ya kusini mwa Asia na mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Heidelberg anasema:
Mashambulio ya kimadhehebu nchini Afghanistan ni njama ya kutaka kudhoofisha serikali na vyombo vya usalama vya nchi hiyo, ili kupitia njia ya kuonyesha kushindwa serikali na idara zake katika kuwalinda raia, suala la uwepo wa vikosi vya kigeni liimarishwe zaidi. Serikali kwa sasa mjini Kabul inakabiliwa na mgawanyiko wa ndani baina ya Rais Ashraf Ghani na Abdallah Abdallah, Mtendaji Mkuu wa serikali ya Afghanistan kuhusiana na suala la kugawana madaraka, suala ambalo limepelekea kujitokeza ukosefu wa usalama wa ndani.
Alaa kulli haal, inaonekana kuwa, sambamba na kuchochea hisia za kikaumu na vita vya kimadhehebu nchini Afganistan, kupatiwa changamoto uwezo na nguvu za vikosi vya usalama nchini humo ni miongoni mwa malengo ya magaidi ili kwa njia hiyo yaonyeshe kwamba, nchi hiyo ingali inahitajia suala la kuendelea kuweko nchini humo vikosi vya kigeni.
Hapana shaka kuwa, makundi ya kigaidi ambayo yanafuatilia malengo yao kwa kuendelea mgogoro nchini Afghanistan, yakipata himaya na uungaji mkono wa washirika wao yatafanya kila yawezalo kuhakikisha kwamba, vurugu na machafuko yanaendelea kushuhudiwa katika nchi hiyo.
Katika mazingira kama hayo, jukumu la jeshi na vikosi vya usalama vya Afghanistan ni zito mno kwa ajili ya kuhitimisha hali ya mchafukoge katika nchi hiyo, na wananchi wa Afghanistan wanataraji kuona kundi la Taliban nalo likisitisha mashambulio yake na hivyo kuisaidia serikali ya Kabul katika juhudi zake za kurejesha amani na utulivu nchini humo.