Sisitizo la EU la kuhifadhiwa ushirikiano wake wa kiuchumi na Iran
Umoja wa Ulaya mara kwa mara umekuwa ukisisitizia haja ya kuimarishwa uhusiano wake na Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na sababu kuu ni nafasi muhimu na bora ya Iran katika eneo la Mashariki ya Kati ikiwa ni pamoja na nafasi yake bora katika upande wa jiopolitiki, kisiasa, kiuchumi na kinishati. Jambo jingine linalopewa umuhimu na Umoja wa Ulaya ni kulinda mapatano ya nyukilia ya JCPOA.
Amma kitendo cha Marekani cha kujitoa katika mapatano hayo mwezi Mei mwaka huu na baadaye kurejesha vikwazo dhidi ya Iran kwa awamu mbili za mwezi Agosti na Novemba 2018 kumeuweka Umoja wa Ulaya kwenye mashinikizo hususan kutokana na ung'ang'anizi wa rais wa Marekani Donald Trump wa kuzitaka nchi za Ulaya zishirikiane naye katika njama zake hizo mpya dhidi ya Iran. Hivi sasa Umoja wa Ulaya unakabiliwa na masuala muhimu, la kwanza ni kuyalinda makubaliano ya nyuklia ya JCPOA na la pili ni kukabiliana na mashinikizo ya Marekani. Hata hivyo inaonekana kuwa Umoja wa Ulaya unastahabu kuyalinda mapatano ya nyuklia na kuimarisha uhusiano wake na Iran sambamba na kukabiliana na mashinikizo ya Washington. Hivi karibuni Mkuu wa Kamisheni ya Umoja wa Ulaya, Jean-Claude Juncker ametangaza waziwazi kuwa EU imeamua kulinda uhusiano wake wa kibiashara na kiuchumi na Iran.
Amesema: Umoja wa Ulaya unashirikiana kwa karibu na wanachama wa umoja huo pamoja na waitifaki wake wengine katika kutafuta njia za kuwezesha kuchukuliwa hatua muhimu za kulinda ushirikiano baina ya Iran na Umoja wa Ulaya katika sekta muhimu mno ya uchumi.
Viongozi wa ngazi za juu wa Umoja wa Ulaya wanaamini kuwa chombo hicho kina wajibu wa kuonesha uaminifu wake katika kipindi hiki kigumu kupitia kuendeleza ushirikiano wake na Iran na kwa njia hiyo uweze kusaidia jitihada za kuimarisha utulivu ulimwenguni. Ni kwa sababu hiyo ndio maana hata baada ya mshirika muhimu wa Ulaya yaani Marekani kutangaza kujitoa kwenye mapatano ya nyuklia ya JCPOA, Umoja wa Ulaya umeamua kuendelea na kuyalinda mapatano hayo.
Tofauti na Marekani inayodai bila mashiko kuwa eti Iran haiheshimu vipengee vya mapatano hayo, Umoja wa Ulaya kwa upande wake unasisitiza kuwa Tehran imeheshimu kikamilifu mapatano hayo na kwamba makubaliano hayo ndiyo njia bora ya kudhibiti shughuli za nyuklia za Iran. Nchi hizo za Ulaya aidha zinasisitiza kuwa mapatano ya JCPOA yameweza kufanikisha malengo yake yaani kuzuia kuzuka mivutano na ugomvi kieneo na kimataifa.
Kwa kweli mtazamo wa Umoja wa Ulaya ni kwamba, JCPOA ni mfano bora wa mapatano ya pande kadhaa ambao unaweza kufanywa muongozo na kigezo cha kutatulia matatizo mengine ya kimataifa.
Ni kwa sababu hiyo pia ndio maana Jean-Claude Juncker akasema hadharani kuwa, madhali Iran itaendelea kuheshimu vipengee vya JCPOA, basi Umoja wa Ulaya nao utaendelea kuheshinmu mpatano hayo hasa kwa kuzingatia kuwa umoja huo ni moja ya wafanikishaji wa JCPOA kwa ajili ya kuleta usalama na amani.
Sisitizo la Umoja wa Ulaya la kulinda uhusiano wake wa kiuchumi na kibiashara na Iran ni sehemu ya matunda ya makubaliano hayo ya nyuklia. Umoja huo umekuwa ukichukua hatua mbalimbali za kuhakikisha kwamba unahifadhi ushirikiano wake wa kiuchumi na kibiashara na Iran ambapo moja ya juhudi hizo ni kubuni njia maalumu ya ubadilishanaji fedha inayojulikana kwa jina la SPV kwa ajili ya kuendeleza miamala ya kifedha, kibiashara na kinishati kati yake na Iran.
Hii ni katika hali ambayo, mara kwa mara viongozi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran wamekuwa wakisisitiza kwamba, sharti lao kuu la kuendelea kuheshimu mapatano ya JCPOA ni kuhisi kuwa ina faida ndani yake na wakati wowote itakapohisi hayaifadishi tena, basi itajitoa kwenye mapatano hayo. Katika matamshi ya hivi karibuni kabisa, Dk Ali Akbar Salehi, Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ambaye pia ni Mkuu wa Taasisi ya Atomiki ya Iran amesema: Kama tutahisi kuwa hatuwezi kuuza mafuta yetu na hatuwezi kustafidi na mabadilishano ya kifehda, wakati huo tena sidhani kwamba kutakuwa tena na faida ya sisi kuendelea kuheshimu vipengee vya mapatano ya JCPOA.
Inaonekana ni kwa kuzingatia tahadhari hizo zinazotolewa na Iran ndio maana Ufaransa na Ujerumani zikatangaza kwamba ziko tayari kuwa wenyeji njia mpya ya mabadilishano ya kifedha baina ya Ulaya na Iran hasa baada ya Luxembourg na Austria kukataa kuwa na wenyeji wa njia hiyo maalumu ya mabadilishano ya fedha.