Ulaya yasisitiza tena kulinda makubalino ya nyuklia ya JCPOA
(last modified Sat, 16 Feb 2019 13:39:36 GMT )
Feb 16, 2019 13:39 UTC
  • Ulaya yasisitiza tena kulinda makubalino ya nyuklia ya JCPOA

Licha ya makubaliano ya nyuklia ya JCPOA kuwa na umuhimu mkubwa katika kudumisha amani na usalama wa kimataifa, lakini Marekani mwezi Mei mwaka jana ilijitoa kwenye makubaliano hayo ili kuyasambaratisha.

Kwa mtazamo wa Ulaya ni kuwa, kitendo cha kuvuruga makubaliano ya nyuklia ya Mpango Kamili wa Pamoja wa Utekelezaji (JCPOA) na kuyafuta kina taathira hasi za kiusalama na wakati huo huo kinatilia shaka pakubwa itibari ya diplomasia ya Ulaya. Brussels kwa upande wake inaamini kuwa makubaliano hayo ya nyuklia ya kimataifa ni mfano wa makubaliano ya pande kadhaa ambayo yanaweza kutumiwa kama kigezo na nembo kwa ajili ya kuipatia ufumbizi mizozo mingine ya kimataifa. Pamoja na hayo, serikali ya Trump katika wiki kadhaa za karibuni khususan baada ya kutangazwa kuanzishwa mfumo maalumu wa biashara baina ya Ulaya na Iran maarufu kama INSTEX, imeshadidisha mashinikizo ya pande tofauti ili kuzilazimisha Umoja wa Ulaya na Troika ya Ulaya inayoundwa na Ujerumani, Ufaransa na Uingereza zisalimu amri na kuamua kujitoa kwenye makubaliano ya nyuklia ya JCPOA. Mashinikizo hayo yamedhihirika pia katika kikao cha karibuni Warsaw ambapo Mike Pence Makamu wa Rais wa Marekani alikosoa vikali misimamo ya Ulaya kuhusiana na makubaliano hayo ya nyuklia. Brian Hook, mkuu wa kundi la uchukuaji hatua dhidi ya Iran katika Wizara ya Mashauri ya Kigeni ya Marekani amesema katika mazungumzo yake na gazeti la al Sharq Ausat kwamba: Marekani na Ulaya zinahitilafiana kuhusu mbinu na namna ya kuamiliana na Iran.  

Brian Hook, Mkuu wa Kundi la Uchukuaji Hatua dhidi ya Iran katika Wizara ya Mashauri ya Kigeni ya Marekani 
 

Wakati huo huo misimamo mipya inayochukuliwa na viongozi wa ngazi ya juu wa Umoja wa Ulaya na Troika ya Ulaya inaashiria azma ya pande hizo kwa ajili ya kuyalinda makubaliano ya JCPOA licha ya mashinikizo hayo yote ya Washington. Federica Mogherini Mkuu wa Siasa za Nje wa Umoja wa Ulaya jana alasiri alisisitiza katika Mkutano wa Usalama huko Munich Ujerumani kuwa: Ulaya itaendelea kutekeleza kikamilifu makubaliano ya nyuklia ya JCPOA licha ya mashinikizo yote hayo. 

Msimamo huo wa Umoja wa Ulaya aidha umethibitishwa na kuungwa mkono na nchi nyingine kubwa za Ulaya. Akizungumza jana usiku katika Mkutano wa Usalama wa Munich, Heiko Maas Waziri wa Mambo ya Nje wa Ujerumani  amepinga wito wa Marekani wa kuitaka Ulaya ijitoe katika makubaliano ya JCPOA. Maas aidha alikosoa hatua ya Marekani ya kujitoa kwenye makubaliano hayo ya nyuklia ya kimataifa na kusisiza kuwa: Ujerumani pamoja na Uingereza na Ufaransa kufikia sasa zimepata njia kadhaa za kulinda na kuyaendeleza makubaliano ya JCPOA. 

Heiko Maas, Waziri wa Mambo ya Nje wa Ujerumani 

Serikali ya Marekani ilianza kutekeleza vizuizi mbalimbali ili kukwamisha utekelezaji wa makubaliano ya nyuklia ya JCPOA sambamba na kufanya jitihada za kuzuia Iran kunufaika kiuchumi na makubaliano hayo tangu kuanza kutekelezwa kwake Januari 16 mwaka 2016. Vizuizi na hila hizo ziliongezeka mara baada ya Donald Trump kuingia madarakani huko Marekani. Akiwa katika kampeni za kuwania kiti cha urais na baada ya kuingia madarakani huko White House; Trump mara kadhaa aliyadhihaki na kuyataja makubaliano hayo ya nyuklia ya kimataifa kuwa ni makubaliano mabaya zaidi kuwahi kufikiwa na kutishia kuwa nchi yake itajitoa kwenye makubaliano hayo. Hatimaye siku ya Jumanne mwezi Mei mwaka jana Trump alikiuka ahadi za Washington mkabala na makubaliano ya JCPOA ambapo alichukua uamuzi wa upande mmoja na kutangaza kuitoa nchi  yake katika makubaliano hayo ya kimataifa na kisha akatangaza kuvirejesha vikwazo vya nyuklia dhidi ya Iran. Kama alivyosema Brian Hook kwa sababu hiyo Washington ilijitoa katika mapatano ya JCPOA; ili ipate kushadidisha mashinikizo dhidi ya Tehran na kuendeleza pia siasa za mashinikizo ya kiwango cha juu dhidi ya Iran. 

Kujitoa Marekani katika makubaliano ya JCPOA kumekosolewa pakubwa kimataifa khususan na nchi zile zilizofikia makubaliano hayo. Nchi wanachama zilizofikia makubaliano hayo ya nyuklia katika kundi la 4+1 zimekuwa zikisisitiza kulindwa makubaliano hayo, kushirikiana na Iran na kutafuta njia mbalimbali ili kupunguza taathira hasi zinazotokana na kurejeshwa tena vikwazo vya Marekani dhidi ya Iran. Katika uwanja huo, Umoja wa Ulaya na Troika ya Ulaya zimeazimia kuwasilisha mfumo maalumu wa fedha ambao utavifanya vikwazo hivyo vya Marekani dhidi ya Iran kutokuwa na taathira kubwa. Tarehe 31 mwezi Januari mwaka huu Umoja wa Ulaya ulitangaza rasmi kuanzisha kanali maalumu ya miamala ya kibiashara kati ya nchi za Ulaya na Iran kwa jina la INSTEX; hatua ambayo japokuwa ina athari chache za kivitendo katika kupunguza madhara ya vikwazo vya Marekani dhidi ya Iran, lakini imeonyesha namna Ulaya ilivyojiimarisha kimfumo kukabiliana na Marekani.  

Tags