Uhispania yapinga kutumwa nchini Syria wanajeshi wa muungano wa Nato
Waziri wa Mambo ya Nje wa Uhispania amepinga ombi la Marekani kwa nchi wanachama wa Muungano wa Kijeshi wa Nchi za Magharibi (Nato) kwa ajili ya kutumwa wanajeshi wa nchi hizo huko Syria.
Josep Borrell amesema kuwa aghalabu ya nchi wanachama wa Nato zinapinga uamuzi huo wa Washington. Waziri wa Mambo ya Nje wa Uhispania ameyasema hayo katika radiamali yake kwa ombi la Marekani iliyotaka kutumwa wanajeshi zaidi huko Syria.
Borrell ameongeza kuwa Uhispania na akthari ya nchi wanachama wa muungano wa Nato haziko tayari kuona wanajeshi wake wanachukua nafasi ya vikosi vya Marekani huko Syria baada ya nchi hiyo kuondoa wanajeshi wake. Mike Pence Makamu wa Rais wa Marekani amezitolea wito nchi za Ulaya kutuma huko Syria wanajeshi hadi kufikia 1500. Makamu wa Rais wa Marekani ameongeza kuwa Washington itaondoa wanajeshi wake elfu mbili huko Syria mkabala na nchi za Ulaya kutuma wanajeshi wao nchini humo. Rais Donald Trump wa Marekani mwezi Disemba mwaka jana alitangaza kuwa ataondoa wanajeshi wa nchi hiyo 2000 walioko Syria.
Mgogoro ulianza huko Syria mwaka 2011 kutokana na hujuma kubwa za makundi ya kigaidi kwa uungaji mkono wa Saudi Arabia, Marekani na waitifaki wao, lengo likiwa ni kubadili mlingano katika eneo kwa maslahi ya utawala wa Kizayuni. Hata hivyo njama zote zimegonga mwamba kutokana na jitihada za jeshi na wananchi wa Syria.