UN yataka misaada ya kibinadamu iondolewe katika vikwazo dhidi ya Iran
https://parstoday.ir/sw/news/world-i52602
Mkuu wa Ofisi ya Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa sanjari na kueleza kusikitishwa kwake na taathira hasi za mafuriko yaliyoua makumi ya watu nchini Iran, ametoa mwito wa kuondolewa misaada ya kibinadamu katika orodha ya vikwazo dhidi ya taifa hili.
(last modified 2025-07-19T07:06:59+00:00 )
Apr 03, 2019 14:55 UTC
  • UN yataka misaada ya kibinadamu iondolewe katika vikwazo dhidi ya Iran

Mkuu wa Ofisi ya Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa sanjari na kueleza kusikitishwa kwake na taathira hasi za mafuriko yaliyoua makumi ya watu nchini Iran, ametoa mwito wa kuondolewa misaada ya kibinadamu katika orodha ya vikwazo dhidi ya taifa hili.

Maria Luiza Ribeiro Viotti ameyasema hayo katika mazungumzo aliyoyafanya kwa njia ya simu na balozi mdogo wa Iran katika Umoja wa Mataifa, Eshaq Al Habib na kubainisha kuwa, UN iko tayari kushirikiana na Iran katika jitihada zake za kufikisha misaada ya kibinadamu kwa waathiriwa wa majanga hayo ya kimaumbile.

Sambamba na kutoa mkono wa pole kwa familia zilizowapoteza wapendwa wao, serikali na taifa la Iran kwa ujumla kutokana na mafuriko hayo, afisa huyo wa ngazi za juu wa Umoja wa Mataifa amesema vizingiti vyote vya kuzuia ufikishwaji wa misaada ya kibinadamu kwa waathiriwa wa mafuriko hapa nchini vinapaswa kuondolewa.

Kwa mujibu wa msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, Bahram Qassemi, Marekani imefunga akaunti za Shirika la Hilali Nyekundu hatua ambayo ina maana ya kufunga mlango wa kutumwa misaada ya nchi tofauti za dunia kwa waathirika wa mafuriko yaliyoyakumba maeneo mbalimbali ya Iran.

Athari za mafuriko mjini Shiraz nchini Iran

Amefafanua zaidi kwa kusema, jamii ya kimataifa na asasi za kimataifa zinatakiwa kuchukua hatua madhubuti za kukomesha mienendo hiyo ya kinyama ya Marekani.

Hii ni katika hali ambayo, idadi ya watu waliopoteza maisha kutokana na mafuriko yaliyosababishwa na mvua kubwa zinazonyesha katika maeneo kadhaa ya Iran imeongezeka na kufikia watu 62.