Mbunge avaa mtandio Bungeni kupinga marufuku ya hijabu Austria
Mbunge mmoja wa kujitegemea huko Austria amevaa mtandio kichwani ndani ya Bunge la nchi hiyo kulalamikia na kupinga muswada tata wa sheria inayotaka kupiga marufuku uvaaji wa hijabu kwa mabinti wa Kiislamu wa shule za msingi katika nchi hiyo ya Ulaya.
Huku akiwa amevaa mtandio kichwani, mwanasiasa huyo kwa jina Martha Bissmann alikiambia kikao cha Bunge cha jana Ijumaa kuwa, "Marufuku hiyo ni ya kibaguzi na yenye lengo la kueneza chuki dhidi ya Waislamu nchini humo. Tusikubali kutenganishwa na kuzozanishwa."
Amesema sheria hiyo inayopiga marufuku watoto wa kike wa shule za msingi zikiwemo za binafsi wenye chini ya umri wa miaka 10 kuvaa hijab ni hujuma kwa 'thamani aali' za nchi hiyo kama kuvumiliana na ukiukaji wa uhuru wa kuabudu.
Katika hali ambayo wabunge wa upinzani waliupinga na kuukashifu muswada huo, wabunge wa vyama vinvyoegemea mrengo wa serikali bungeni waliuunga mkono. Miongoni mwa wabunge waliouunga mkono muswada huo ni wale wa chama tawala cha kihafidhina cha ÖVP cha Chansela wa nchi hiyo, Sebastian Kurz na kile kinachopinga uwepo wa wahamiaji nchini humo cha FPO.

Wakati huohuo, Muungano wa Jamii ya Waislamu nchini humo (IGGOe) umetoa taarifa ya kupinga sheria hiyo, ukisisitiza kuwa marufuku hiyo ya hijabu kwa watoto wa shule za msingi ni fedheha na ubaguzi.
Oktoba mwaka 2017, serikali ya Austria ilianza kutekeleza rasmi marufuku ya wanawake Waislamu kuvaa hijabu inayofunika uso wote maarufu kama burqa au niqabu katika maeneo yote ya umma nchini humo.
Kwa mujibu wa utafiti uliofanywa na Kituo cha Ushauri kwa Waislamu Austria, kati ya watu milioni tisa nchini humo, takribani laki 7 ni Waislamu.