Madai ya Waziri wa Mambo ya Nje wa Ujerumaini kuhusu JCPOA
Umoja wa Ulaya na troika ya umoja huo inayoundwa na Ujerumani, Ufaransa na Uingereza daima imekuwa ikidai kuwa inaunga mkono mapatano ya nyuklia na Iran maarufu kwa jina la JCPOA na kwmba nchi hizo zimekuwa zikisisitizia muda wote umuhimu wa kutekelezwa kivitendo mapatano hayo.
Hata hivyo baada ya Marekani kujitoa katika makubaliano hayo ya kimataifa mwezi Mei 2018, Umoja wa Ulaya umepata kisingizio cha kuchelewesha utekelezaji wa ahadi zake, suala ambalo limeilazimisha Iran nayo kupunguza kiwango cha ahadi zake ndani ya JCPOA. Hivi sasa Umoja wa Ulaya umekumbwa na changamoto kubwa ya kuweza kuyalinda makubaliano hayo muhimu sana kwa usalama na amani duniani.
Msimamo wa karibuni kabisa wa nchi za Ulaya kuhusu JCPOA ni matamshi ya Heiko Maas, Waziri wa Mambo ya Nje wa Ujerumani. Sambamba na kuashiria kwamba ni vigumu sana kwa Iran kuweza kufaidika na matunda ya kiuchumi ya JCPOA, waziri huyo wa mambo ya nje wa Ujerumaini amedai kuwa: Ulaya inatekeleza ahadi zake ndani ya mapatano ya JCPOA, jambo ambalo linatarajiwa pia lifanywe na Iran.
Ukweli wa mambo ni kuwa, Waziri wa Mambo ya Nje wa Ujerumaini inaonekana amekusudia kuifanya Ulaya isitekeleze ahadi zake. Nchi za Ulaya zimeonesha kivitendo kuwa haziko tayari kugharamia utekelezaji wa ahadi zao ndani ya JCPOA. Ijapokuwa Umoja wa Ulaya unaamini kuwa mapatano ya JCPOA yanalinda manufaa makubwa ya barani Ulaya hasa suala la usalama na amani katika eneo nyeti la Asia Magharibi na kimataifa, lakini pamoja na hayo, Waziri wa Mambo ya Nje wa Ujerumaini amejitokeza na kudai kuwa ni vigumu kwa Iran kuweza kupata manufaa ya kiuchumi ndani ya JCPOA. Amesema: Baada ya mwaka mzima wa kujitoa Marekani kwenye JCPOA, ni wazi kuwa si rahisi kuyalinda mapatano hayo. Manufaa ya kiuchumi iliyoahidiwa Iran ndani ya JCPOA yamekumbwa na uzito wa utekelezaji baada ya Marekani kujitoa kwenye mapatano hayo. Hata hivyo tungali tunapigaia jambo hilo. Dunia imekuwa na usalama na amani zaidi kwa kuwepo mapatano hayo na si kinyume chake.
Waziri wa Mambo ya Nje wa Ujerumani amedai kuwa Ulaya imetekeleza ahadi zake katika JCPOA. Lakini licha ya madai hayo, hivi sasa zaidi ya mwaka umeshapita tangu Marekani ijitoe kwenye mapatano hayo na bado Umoja wa Ulaya pamoja ya troika yake ya Ujerumani, Ufaransa na Uingereza hazijaweka mkakati wowote wa maana wa kutekeleza kivitendo ahadi zao ukiwemo mfumo maalumu wa mabadilishano ya kifedha na kibiashara baina ya Ulaya na Iran maarufu kwa jina la INSTEX. Kuzembea nchi za Ulaya kutekeleza ahadi zao ndiko kulikoilazimisha Iran nayo ichukue hatua kwa mujibu wa mapatano ya JCPOA. Mwanzoni mwa mwezi Aprili 2019 Iran ilitangaza kuwa inapunguza kiwango cha ahadi zake ndani ya JCPOA na ilitoa muda wa siku 60 kwa nchi za Ulaya kuhakikisha zinatekeleza ahadi zao kabla ya Tehran kuchukua hatua nyingine. Katika sehemu moja ya matamshi yake, Waziri wa Mambo ya Nje wa Ujerumani ametoa matamshi ya kuwapotosha walimwengu ili wasizingatie jinsi Ulaya ilivyoshindwa kutekeleza ahadi zake ndani ya JCPOA. Amesema: Tunafanya jitihada za kuyalinda mapatano ya JCPOA kwa sababu hatuna imani na Iran.
Amma swali linalojitokeza hapa ni kuwa, je ni Iran ndiyo isiyoaminika au ni nchi za Ulaya ambazo kwa zaidi ya mwaka sasa tangu ijitoe Marekani kwenye JCPOA zimeshindwa kutekeleza ahadi zao? Majibu yake ni kwamba tangu yalipoanza kutekelezwa mapatano ya JCPOA, Iran imetekeleza kikamilifu ahadi zake ndani ya mapatano hayo. Uhakika huo unathibitishwa na ripoti 14 za Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki ambazo zimesema kwa yakini kwamba Iran imetekeleza kikamilifu ahadi zake. Hivyo nchi za Ulaya hazina kisingizio chochote cha kukwepa kutekeleza ahadi zao.
Hivi sasa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imetoa muda wa siku 60 kwa nchi za Ulaya kuhakikisha zinaheshimu mapatano ya JCPOA na zinatekeleza kivitendo ahadi zao. Lakini kama Ulaya itaendelea kupoteza muda na kujichelewesha katika kutekeleza vipngee vya makubaliano ya JCPOA, basi nchi za Ulaya zisiwe na matumaini kwamba Tehran nayo itaendelea kujifunga na vipengee vya makubaliano hayo.