Mshauri wa Erdogan amuonya Mfalme wa Saudia dhidi ya kuwanyonga wanazuoni
Mshauri wa Rais Recep Tayip Erdogan wa Uturuki amemuandikia barua Mfalme Salman Bin Abdulaziz Aal-Saud wa Saudi Arabia, akimtahadharisha juu ya matokeo mabaya ya mpango wa utawala wake wa kuwanyonga wanazuoni watatu mashuhuri nchini humo baada ya mwezi mtukufu wa Ramadhani.
Yasin Aktay amemuandikia Mfalme wa Saudia barua hiyo ya wazi iliyochapishwa na gazeti la Uturuki la Yeni Şafak ambapo amebainisha kuwa, "Mfalme wa Saudia hatapata chochote kwa kutekeleza hukumu hiyo isipokuwa matatizo. Wanazuoni ni warithi wa Mitume na kifo cha mwanachuoni mmoja ni sawa na kifo cha dunia yote, kama ambavyo mauaji ya msomi mmoja ni sawa na mauaji ya wasomi wote duniani."
Mshauri huyo wa Rais wa Uturuki ameeleza bayana kuwa, kadhia ya wasomi sio suala la ndani ya Saudia, bali ni jambo linalouhusu umma wote wa Kiislamu, na kwamba kosa tu la kuwazuilia achilia mbali kuwanyonga, linaweza kuharibu maisha yote.
Hivi karibuni, tovuti ya habari ya Middle East Eye yenye makao makuu yake mjini London iliripoti kuwa, watawala wa Riyadh wamepanga kuwanyonga wanazuoni hao mashuhuri ambao ni Sheikh Salman al-Ouda, Sheikh Awad al-Qarni na Ali al-Omari baada ya mwezi mtukufu wa Ramadhani, kwa tuhuma bandia za ugaidi.
Mauaji hayo ni katika muendelezo wa ukatili na ukandamizaji dhidi ya wasomi, wapinzani na wakosoaji wa utawala wa Aal-Saud unaoongozwa na Mrithi wa Kiti cha Ufalme wa utawala huo, Mohammed bin Salman.
Sheikh Ouda ni Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Kimataifa ya Wanazuoni wa Kiislamu, ambayo Riyadh imeiweka katika orodha yake ya mashirika ya kigaidi. Wataalamu wa Umoja wa Mataifa wanamfahamu mwanazuoni huyo kama mwanamageuzi.
Sheikh al-Qarni pia ni mwanachuoni mashuhuri nchini Saudia, mwanaakademia na mwandishi mtajika, na al-Omari ni mtangazaji mashuhuri wa Kiislamu nchini humo.